2015-01-28 12:28:49

Mchakato wa kumtangaza Chiara Lubich kuwa Mwenyeheri waanza!


Askofu Raffaelo Martinelli wa Jimbo Katoliki la Frascati, Italia, tarehe 27 Januari 2015 ameratibu kikao cha kwanza katika mchakato wa kumtangaza mtumishi wa Mungu Chiara Lubich, kuwa Mwenyeheri na hatimaye, Mtakatifu, tukio ambalo limeshuhudiwa na umati mkubwa wa waamini kutoka ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Frascati.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na kusomwa na Kardinali Tarcisio Bertone, aliyekuwepo kwenye tukio hili, anamsifu Mtumishi wa Mungu Chiara Lubich, mwanzilishi wa Chama cha Kitume cha Wafokolari na kwa wale wote ambao wanaendeleza karama ya maisha ya kiroho, hazina na urithi mkubwa ulioachwa na Mtumishi wa Mungu.

Baba Mtakatifu anawatakia neema na baraka wale wote wanaoendesha mchakato wa kutangazwa kwake kuwa Mwenyeheri, kuisaidia Familia ya Mungu, kazi na utume uliotekelezwa na Chiara Lubich katika maisha yake hapa duniani, ili kupokea mwanga mpya unaolichangamotisha Kanisa kujikita katika umoja kamili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.