Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara, katika mahojiano maalum
na Radio Vatican anabainisha umuhimu wa mshikamano wa dhati katika maisha ya ndoa
na familia kwa kutambua kwamba, familia ni mahali pa kutakatifuza maisha ya mwanadamu,
shule ya kwanza upendo, haki na amani.
Familia ni
mahali pa kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu; yote haya yanawezekana
ikiwa kama wazazi wa pande zote mbili wanatekeleza dhamana na wajibu wao wa kulea
na kuwafunda watoto wao!
Askofu Niwemugizi anasema kwamba, familia nyingi nchini
Tanzania zinakabiliwa na changamoto mbali mbali za maisha hususan katika uwanja wa
malezi bora; dhamana inayopaswa kutekelezwa na wazazi wa pande zote mbili, lakini
leo hii kuna familia nyingi ambazo ni tenge, yaani kuna mzazi mmoja anayewajibika
katika yote, hali ambayo inakwamisha malezi kwa watoto.
Hali ngumu ya maisha
imepelekea familia nyingi kujikuta zinaogelea katika lindi la umaskini wa hali na
kipato, kiasi hata cha kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kulea na kuwafunda
watoto; wazazi wengi wanashindwa kuzihudumia familia zao kwa kuzipatia mahitaji msingi,
matokeo yake ni baadhi ya wazazi, hasa akina baba kutelekeza familia zao na "kuishia
mitini".
Baadhi ya familia zinashindwa kujitosheleza kwa mahitaji yake msingi
na matokeo yake, watoto wanalazimishwa kufanya kazi ambazo ni ngumu ikilinganishwa
na umri wao, kiasi cha kuwadumaza katika makuzi yao. Baadhi ya wazazi wamekuwa ni
chanzo cha kuwatumbukiza watoto wao katika biashara mamboleo, ili kusaidia kuchangia
gharama za maisha kwenye familia, matokeo yake ni mimba za utotoni, ongezeko la ugonjwa
wa Ukimwi pamoja na vifo.
Ukosefu wa mshikamano na mfungamanisho wa maisha
ya ndoa na familia pamoja na sababu nyingi, watoto wengi wamejikuta wakiishi katika
mazingira hatarishi. Zote hizi ni changamoto zinazoendelea kuikabili Familia ndani
na nje ya Tanzania. Kuna haja kwa Mama Kanisa kuibua mbinu mkakati utakaoziwezesha
familia kufungamana na hatimaye, kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara kwa ajili
ya ustawi na maendeleo ya Kanisa na Jamii kwa ujumla, hasa wakati huu, Mama Kanisa
anapijielekeza katika mchakato wa kuwatangazia Watu wa Mataifa, Injili ya Familia.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.