2015-01-27 09:23:36

Kanisa nchini Vietnam ni moto wa kuotea mbali!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye amehitimisha hija yake ya kichungaji nchini Vietnam anasema kwamba, Vietnam imebarikiwa kuwa na umati mkubwa wa Mapadre na Watawa, wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani katika medani mbali mbali za maisha.

Waamini walei, ni watu wenye ibada na upendo mkubwa kwa Kanisa na Wakleri wanaowahudumia. Ni kundi ambalo linaendelea kushikamana na Kanisa katika maisha na utume wake. Kuna ushirikiano mkubwa kati ya Kanisa na Serikali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, utume unaotekelezwa na Balozi wa Vatican asiye mkazi nchini humo, unaendelea kuimarisha mahusiano kati ya Vietnam na Vatican.

Vietnam ni nchi ambayo inaendelea kucharuka katika medani mbali mbali za maisha, changamoto ya kuendeleza na kukuza majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali nchini humo, sanjari na kukoleza moyo na ari ya kimissionari bila kusahau umuhimu wa utamadunisho, ili kweli Injili ya Kristo, iweze kuota mizizi katika maisha na tamaduni za wananchi wa Vietnam. Idadi ya Wakristo inazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka nchini Vietnam, hili pia anasema Kardinali Filoni, ni jambo la kumshukuru Mungu.

Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo linapenda kuwekeza zaidi na zaidi Barani Asia kama alivyokwishawahi kusema Mtakatifu Yohane Paulo II. Hii ni dhamana inayotekelezwa kwa kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene; haki na amani. Waamini wa Vietnam wanamwomba Baba Mtakatifu Francisko, siku moja kuwatembelea ili aweze kuwaimarisha katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita kwa namna ya pekee kabisa katika ushuhuda wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.