Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu,
mwishoni mwa juma, tarehe 24 Januari 2015 ametembelea na kuadhimisha Ibada ya Misa
takatifu katika Jimbo Katoliki la Xuan Loc, ambalo lilianzishwa kunako tarehe 14 Oktoba
1965 na Mwenyeheri Paulo VI, ili kurahisisha huduma za kichungaji kwa waamini waliokuwa
wanaongezeka kwa kasi kubwa.
Kumbe, Ibada hii ya Misa Takatifu, ilikuwa ni
kilele cha maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu Jimbo hili lililipoanzishwa. Katika
kipindi cha miaka mitano ya maandalizi ya Jubilee, familia imepewa kipaumbele cha
kwanza, katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kuhakikisha kwamba, familia inakuwa
kweli ni shule ya Neno la Mungu na kwamba, Familia zinajichotea nguvu na neema ya
kusonga mbele katika Sakramenti za Kanisa; kielelezo cha mshikamano wa dhati kati
ya Wakleri na waamini walei.
Mama Kanisa anasema Kardinali Filoni anaendelea
kuwachangamotisha waamini nchini Vietnam kusonga mbele kwa kujikita katika mchakato
wa Uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani katika matendo. Ikumbukwe
kwamba, Jimbo Katoliki la Xuan Loc ni matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican,
linalotegemewa kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji wa Familia ya Mungu kama Mababa
wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanavyokazia.
Ni dhamana ya kuhakikisha
kwamba, Familia ya Mungu inajitahidi kupyaisha imani inayojikita katika matendo yanayoshuhudiwa
katika uhalisia wa maisha ya waamini, daima wakijitahidi kuwa kweli ni waaminifu kwa
Mungu na Kanisa, wakiendelea kukumbatia Injili ya Huruma ya Mungu ili kuwatangazia
jirani zao matendo makuu ya Mungu katika maisha yao. Familia ya Mungu, iwaonjeshe
wengine huruma na upendo wa Mungu kwa kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu na kutangaza
Mwaka wa Bwana.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya
Radio Vatican.