2015-01-26 11:50:16

Wanawake wamesaidia sana kurithisha imani!


Imani ni zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, dhamana inayotekelezwa kwa uchaji mkubwa na wanawake. Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican siku ya Jumatatu, 26 Januari 2015 wakati Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha kumbu kumbu ya Watakatifu Timotheo na Tito.

Baba Mtakatifu anasema, kuna tofauti kubwa ya kufundisha masuala ya imani, lakini imani kimsingi ni zawadi ya Roho Mtakatifu ambayo imekuwa ikifanyiwa kazi na wanawake wachamungu ndani ya familia, kwa kutambua kwamba, Bikira Maria amewazawadia walimwengu Mtoto Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kwake Bikira Maria.

Hivi ndivyo alivyopenda Yesu, ili aweze kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kumbe, imani inarithishwa kwa njia ya wanawake na kwamba waamini wanachangamotishwa kuhakikisha kwamba, wanailinda na kuendelea kuiimarisha kwa njia ya Roho Mtakatifu, vinginevyo imani inaweza kugeuzwa kuwa ni sehemu ya utamaduni.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, wanaachana na tabia ya woga na kamwe wasiionee imani aibu, bali kusimama kidete ili kuweza kuishuhudia na kuiimarisha kwa njia ya paji la nguvu, upendo na hekima, kwa kuwa na kiasi. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Mwenyezi Mungu ili awasaidie kuwa na imani thabiti.







All the contents on this site are copyrighted ©.