Yesu alianza kuhubiri Habari Njema ya Wokovu mara baada ya Yohane Mbatizaji kufungwa
gerezani na Mfalme Herode. Huu ulikuwa ni wakati ambapo sauti ya kinabii ilikuwa inaanza
kutangaza kuhusu Ufalme wa Mungu, lakini Mfalme Herode akamua kuizima. Yesu ndiye
kiini na Habari Njema, utilimifu wa maagano kati ya Mungu na mwanadamu; ndiye Habari
Njema inayopaswa kuaminiwa, kupokelewa na kutangazwa kwa Watu wa nyakati zote, ili
aweze kuaminiwa na wote.
Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu
Francisko wakati wa sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro mjini Vatican, siku ya Jumapili tarehe 25 Januari 2015, siku ya kufunga juma
la kuombea Umoja wa Wakristo.
Baba Mtakatifu anasema, Yesu Kristo ni Neno wa
Mungu aliye hai na anayetenda katika historia, kwa mtu anayemsikiliza na kumfuasa
anaingia kwenye Ufalme wa Mungu. Yesu ni utimiliufu wa ahadi za Mungu kwani anawakarimia
waja wake Roho Mtakatifu. Yesu ni maji hai yanayozima kiu ya moyo wa mwanadamu unaohitaji:
maisha, upendo, uhuru na amani; ni moyo wenye kiu ya Mungu. Ndiyo maana kauli mbiu
iliyoongoza juma la kuombea umoja wa Wakristo kwa Mwaka huu, ilikuwa “nipe maji ninywe”.
Baba
Mtakatifu anasema, Kanisa bado linaendelea kumwomba Kristo ili aweze kulipatia nguvu
na dhamana ya kutafuta umoja kamili kati ya Wakristo, ili wote waweze kuwa wamoja.
Dhambi za Wakristo na historia yao, imekuwa ni chanzo cha utengano, ndiyo maana Wakristo
wanapaswa kuendelea kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwajalia tena umoja.
Baba
Mtakatifu anasema, kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu amekuwa ni kiu ya
binadamu anayetaka utimilifu wa maisha yasiyojikita katika utumwa wa dhambi na mauti.
Kwa hakika, Mwenyezi Mungu ana kiu na upendo wa mwanadamu unaojikita katika Moyo Mtakatifu
wa Yesu, ambao kimsingi ni daraja kati ya kiu ya Mungu na mwanadamu. Yesu anataka
kuunganisha, lakini Shetani daima amekuwa ni chanzo cha migawanyo, chuki na vita.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.