Yesu katika maisha na utume wake, kamwe hakusita kukutana na kuzungumza na watu ambao
walikuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, kiasi hata cha kukutana na kuzungumza
na mwanamke Msamaria na hivyo kuanzisha majadiliano yaliyopelekea hija ya toba na
wongofu wa ndani. Yesu alionesha uvumilivu mkuu na kumheshimu yule mwanamke Msamaria.
Akawa tayari kujifunua kwake taratibu kama mawio ya jua, kwa kujikita katika upendo
na ukweli; kwa kuonesha ukarimu sanjari na kusikiliza kwa makini. Umoja wa Wakristo
unajengeka kwa njia ya hija ya maisha ya Wakristo pasi na kukata tamaa!
Hayo
yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri kwenye Masifu ya Jioni, Siku
kuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume wa mataifa na siku ya mwisho ya kufunga
sala kwa ajili ya juma la kuombea umoja wa Wakristo. Mwenyezi Mungu anasema Baba Mtakatifu
kadiri ya Maandiko Matakatifu anapaswa kuabudiwa katika roho na ukweli. Leo hii, bado
wakristo wamegawanyika kutokana na historia waliyorithi huko nyuma, changamoto ya
kuvuka vikwazo vyote hivi na kuanza mchakato wa kushiriki katika Fumbo la Upendo linalojikita
katika Utatu Mtakatifu.
Baba Mtakatifu anasema umoja wa Wakristo hauwezi kujengwa
kwa majadiliano ya kiekumene peke yake, bali Wakristo wanapaswa kutambua kwa kina
Fumbo la Mungu na kwamba, wanategemeana, kumbe Wakristo wanaweza kukutana na kujadiliana
kwa pamoja chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, anayesawazisha tofauti na kushinda
kinzani, ili kupatanisha tofauti zinazojitokeza.
Yesu anajionesha kuwa ni chemchemi
hai inayozima kiu ya maisha ya mwanadamu; kiu ambayo inajikita katika ukweli, upendo,
haki na uhuru na kwamba, kwa njia ya Fumbo la Pasaka, Yesu anakata kiu yote ya maisha
ya binadamu, pale Moyo wake Mtakatifu unapotobolewa na hivyo kutoa Damu na Maji, kielelezo
cha hali ya juu cha upendo wa Mungu kwa binadamu, changamoto ya kujenga na kudumisha
umoja wa Watoto wa Mungu, unaojikita katika unyenyekevu wa Kristo.
Baba Mtakatifu
anasema, Yesu kwa kukutana na Mwanamke Msamaria, anamsaidia kuwa Mmissionari, anaacha
yote aliyokuwa nayo pale kisimani na kuanza kutimua mbio kwenda mjini ili kuwashirikisha
wengine ile furaha ya kukutana na Yesu katika maisha yake. Leo hii kuna kundi kubwa
la watu waliochoka na wenye kiu ya kumwona Mungu, changamoto ya kuendeleza mchakato
wa Uinjilishaji, kwa Makanisa kushirikiana kwa karibu zaidi pamoja na kuvuka kishawishi
cha kutaka kuwaongoa watu na mashindano yasiokuwa na tija wa la mashiko.
Baba
Mtakatifu anasema, kuna Wakristo wanaoendelea kudhulumiwa, kunyanyaswa na hatimaye
kuuwawa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hawa ni mashuhuda wa Kristo,
wanauwawa hata pasi ya kuulizwa wanatoka katika madhehebu gani; wanauwawa kwa vile
ni Wakristo, huu ndio uekumene wa damu.
Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza
wawakilishi mbali mbali wa madhehebu ya Kikristo walioshiriki katika Ibada ya kufunga
rasmi juma la kuombea umoja wa Wakristo bila kuwasahau watawa kutoka katika Makanisa
mbali mbali waliokuwa wanashiriki katika kongamano la Mwaka wa Watawa Duniani mintarafu
mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Watawa wa madhehebu mbali mbali ya Kikristo
wanapaswa kufahamiana na kushirikishana uzoefu, ujuzi na mang'amuzi, ili kuendelea
kulipyaisha Kanisa.
Baba Mtakatifu anasema,Wakristo wana kiu ya amani na udugu,
changamoto ya kuendelea kuliomba Fumbo la Utatu Mtakatifu, Bikira Maria, Mitume na
Watakatifu wote, ili Wakristo waweze kupata zawadi ya umoja, ili kweli Fumbo la Umoja
wa Kanisa liweze kung'ara.
Naye Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa
la kuhamasisha umoja wa Wakristo, amemwambia Baba Mtakatifu kwamba, Wakristo wa madhehebu
mbali mbali wamekusanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, nje ya kuta za Roma,
ili kuomba maji ya uzima wa milele, kwa kutambua kwamba, kwa njia ya Maji ya Ubatizo,
Wakristo wamefanywa kuwa wamoja katika Yesu Kristo na kwamba, Ubatizo ni Sakramenti
ya Umoja na amani, ili kuvuka chuki, kinzani na vita. Wakristo wanachangamotishwa
na Mama Kanisa kuwa kweli ni vyombo vya amani na upatanisho, mwaliko wa kutubu na
kumwongokea Kristo, tayari kuwa Wamissionari wa Kristo kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu
Paulo, Mwalimu wa Mataifa.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.