Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 25 Januari 2015, kwenye Uwanja
wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko anasema,
anaendelea kufuatilia kwa wasi wasi mkubwa machafuko ya kisiasa yanayoendelea kutendeka
nchini Ucrain; mambo ambayo yanaendelea kusababisha umwagaji wa damu ya raia wasiokuwa
na hatia.
Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wote kwamba, yuko karibu
nao kwa njia ya sala na anapenda kutoa mwaliko kwa wahusika wakuu, kuanzisha tena
mchakato wa majadiliano ili kusitisha chuki, uhasama na vita vinavyoendelea nchini
humo.
Baba Mtakatifu Francisko, amewakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi
mema kwamba, Jumapili, ilikuwa ni Siku ya Wagonjwa wa Ukoma Duniani. Anapenda kuonesha
uwepo wake wa karibu kwa wagonjwa wa ukoma, wale wanaowahudumia pamoja na wataalam
wanaoendelea kujisadaka mchana na usiku ili kuweza kupata tiba ikayaoweza kuwarudia
wagonjwa wa ukoma hadhi yao.
Baba Mtakatifu Francisko, amewashukuru kwa namna
ya pekee kabisa Jumuiya ya wananchi wa Ufilippini, waliokuwa wamekusanyika kwa wingi
wakiwa wanapeperusha bendera ya nchi yao, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anawashukuru kwa ushuhuda wa imani na kazi kubwa
wanayoitenda kwa wakazi wa Roma.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.