Vijana wanapaswa kufundwa kuwapenda na kuwathamini jirani zao kama sehemu ya mchakato
wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu. Jumapili iliyopita, tarehe
25 Januari 2015, wanachama 3, 000 wa Chama cha Vijana Wakatoliki Italia, A.C.R. walifanya
maandamano ya kuombea amani sehemu mbali mbali za dunia na baadaye nyakati za mchana
kuhudhuria kwenye Sala ya Malaika wa Bwana, iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko
kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kauli mbiu ya mwaka
huu ni "Changia amani".
Vijana hao katika ujumbe uliosomwa kwa niaba yao na
kijana Sara wamemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wana kiu ya amani, furaha
na utulivu wa ndani unaopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo na kwamba, kila mwaka
walezi wao wanajibidisha kuwafunda mbinu za kujenga, kulinda na kudumisha amani, kwa
kuchota uzoefu wao kutoka katika hekima, lakini zaidi katika Maandiko Matakatifu.
Vijana
wamekusanya fedha kwa ajili ya kugharimia mradi wa maji utakosaidia wananchi wengi
vijijini nchini Burkina Faso. Maji haya pamoja na matumizi ya nyumbani yatasaidia
pia katika kilimo cha umwagiliaji, ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.