2015-01-26 10:37:47

Huduma katika haki!


Imekwishagota miaka kumi tangu Mama Kanisa alipochapisha Waraka wa kichungaji kuhusu utu wa wanandoa, "Dignitas Connubii", inayojadili kwa kina na mapana changamoto na matatizo katika maisha ya ndoa na familia. Hivi karibuni, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian kiliandaa kongamano la kimataifa kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Sheria za Kanisa, ili kuangalia kwa pamoja dhamana ya wanandoa, ili kuweza kuyasaidia Makanisa mahalia kutoa maamuzi makini kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wanandoa.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na wajumbe hawa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, alikazia umuhimu wa wafanyakazi katika mahakama za Kanisa, kujitahidi kufahamu maagizo yaliyomo kwenye Waraka huu, ili waweze kutekeleza dhamana hii kwa ufanisi mkubwa zaidi, kwa kuwa na uhakika wa kimaadili pamoja na kutoa maamuzi kwa wakati wake badala ya kusubiri kwa muda mrefu, hali ambayo inawachosha wanandoa.

Baba Mtakatifu anawaambia washiriki wa kongamano hili kwamba, jambo la kwanza ni kuhakikisha kwamba, wanalinda na kudumisha vifungo vya maisha ya ndoa na familia na kwamba, Mahakama kuu ya Kanisa Katoliki inaweza kutekeleza wajibu huu nyeti kwa kutamka kwa uhakika kuhusu ndoa inayojadiliwa.

Kwa upande wake Padre Francois- Xavier Dumortier, Mkuu wa Chuo kikuu cha Kipapa cha Gregorian, kilichoko Roma anasema kwamba, huduma ya haki ni dhamana ya kitume, kwa kutambua kwamba, Kanisa linainjilisha na kutoa haki. Wajumbe wa kongamano hili wamemhakikishia Baba Mtakatifu sala zao hasa wakati huu Mama Kanisa anapojiandaa kwa ajili ya Maadhimishio ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.