Familia ya Mungu nchini Tanzania imeshauriwa kuendelea kujituma na kuwekeza zaidi
katika elimu ili iweze kulitumikia vyema Kanisa mahalia kwa kutumia kikamilifu karama
walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa kutambua kwamba, elimu haina mwisho. Wito
huo umetolewa hivi karibuni na Padre Sebastian Mwaja ambaye ni Paroko wa Kanisa kuu
la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo kuu la Dodoma, wakati wa hafla fupi ya kumpongeza
Padre Abel Mwenda na mwanafunzi mwenzake Alpha Muhulo kwa kuhitimu shahada ya elimu
katika Chuo kikuu huria mjini Dodoma. Paroko Mwaja amesema elimu ni urithi na mtaji
pekee wa kujivunia na kwamba endapo waamini, watawa na Wakleri watajituma katika kujiendeleza,
Kanisa litaendelea kudumu katika misingi yake itakayokuwa inaendelea kwa kasi kutokana
na kila mmoja kuchangia karama yake katika kuliendeleza Kanisa mahalia. “Mimi nakupongeza
sana Baba Padre Abel kwa kujituma na kuonesha jihada za kujiendeleza pamoja na mwenzako
hadi mmehitimu, ni tukio la kipekee ambalo kila mmoja wetu katika Jimbo kuu la Dodoma
tuna kila sababu ya kusherehekea na kujivunia,” alisema. Kwa upande wake, Padre
Abel Mwenda amewashukuru mapdre na masista kwa kumtia moyo katika kipindi chote cha
masomo na kwamba, waendelee na moyo huo kwa wengine huku Apha Muhulo akimshukuru Padre
kwa kusaidiana naye katika dhiki na faraja hadi wamehitimu shahada ya kwanza ya elimu. Na
Thompson Mpanji, Dodoma.