2015-01-24 08:02:09

Tutembee kwa pamoja kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia!


Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, hati ya kutendea kazi, "Instrumentum Laboris" kwa ajili ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, inatarajiwa kuwa imekamilika mwishoni mwa mwezi Mei, tayari kuchapishwa mwanzoni mwa mwezi Juni, 2015.

Kardinali Baldisseri ameyasema hayo, Alhamisi, tarehe 22 Januari 2015 wakati alipokuwa anashiriki katika kongamano la vyama vya kitume vya kifamilia kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kwa pamoja kuweza tena kusoma mada mbali mbali zitakazochambuliwa na Mababa wa Sinodi wakati wa maadhimisho ya Sinodi kwa ajili ya familia, hapo mwezi Oktoba 2015.

Maswali dodoso yaliyotumwa kwenye Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, yanapaswa kuwa yamekwishapatiwa majibu na kutumwa kwenye Sekretarieti ya Sinodi za Maaskofu ifikapo tarehe 14 Aprili 2015, tayari kuandaa hati ya kutendea kazi. Wakati wa maadhimisho ya Sinodi, makundi maalum yatapewa dhamana ya kupembua kwa kina na mapana mada kuu tatu ambazo hazikupata ridhaa kubwa kutoka kwa wajumbe waliokuwa wanahudhuria maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kuhusu familia, iliyofanyika mjini Vatican, Mwezi Oktoba 2014.

Ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema kipindi hiki kwa kushirikisha mawazo na mang'amuzi yao kuhusu familia, ili kuliwezesha Kanisa kutangaza Injili ya Familia kwa ari na moyo mkuu zaidi. Baadhi ya wajumbe watakaoshiriki katika Tume itakayoshughulikia mchakato wa kutengua ndoa ya Kikristo, tayari wamekwisha teuliwa na Baba Mtakatifu Francisko. Baadhi ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki tayari yamekwishaanza kutuma orodha ya wajumbe watakaoshiriki katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia.

Wajumbe wa vyama vya kitume kuhusu familia, wamehamasishwa hata wao kujaza maswali dodoso na kutuma majibu yao kwa Sekretarieti ya Sinodi za Maaskofu, ili yaweze kufanyiwa kazi, tayari Kanisa liweze kuwasaidia waamini kushiriki vyema katika maisha na utume wa Kanisa. Mada nyeti zilizopembuliwa na Mababa wa Sinodi, zinapaswa kushughulikiwa kikamilifu, ili hatimaye, Kanisa liweze kufanya maamuzi yenye ujasiri kwa ajili ya kuganga na kutibu familia ambazo zina madonda makubwa katika maisha yao.

Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia anasema, vyama vya kitume ni matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na vimechangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta dira na mwelekeo mpya katika maisha na utume wa Kanisa. Mchango kutoka kwa waamini walei ni mchakato mpya ambao Baba Mtakatifu anapenda kuufanyia kazi mintarafu maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu, ili kuweza kupata majibu muafaka badala ya maamuzi mazito kutolewa uamuzi na viongozi wachache wa Kanisa.

Kanisa linaandaa maadhimisho ya Sinodi ya waamini walei, ili kutoa dira na mwelekeo kwa siku za usoni, kwa njia ya ushuhuda wa kinabii unaopania kuyatakatifuza malimwengu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.