Baba Mtakatifu Francisko ameiandikia Familia ya Mungu nchini Malawi, ujumbe wa upendo
na mshikamano hasa wakati huu inapokabiliana na janga la mafuriko ambalo limeathiri
maisha ya watu na miundo mbinu. Katika ujumbe uliotiwa sahihi na Kardinali Pietro
Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Thomas Msusa wa Jimbo kuu la
Blantyre, Malawi, Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wananchi wote wa Malawi walioguswa
na mafuriko haya uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala.
Baba Mtakatifu anawaombea
ujasiri na nguvu ya kukabilia na changamoto zilizopo kwa sasa na kwamba, anatumaini
kuwa Jumuiya ya Kimataifa itawasaidia wananchi wa Malawi katika kipindi hiki kigumu.
Anawatakia kheri na baraka wafanyakazi wote wanaoendelea kutoa huduma mbali mbali
kwa waathirika wa mafuriko yaliyotokea hivi karubuni nchini Malawi.
Wakati
huo huo, Rais Peter Mutharika wa Malawi ametangaza kwamba, kuna Wilaya kumi na tano
ambazo zimekumbwa na mafuriko na zinahitaji msaada wa dharura. Takwimu zinaonesha
kwamba, kuna zaidi ya watu 200 ambao wamefariki dunia na wengine wengi hawana mahali
pa kuishi kutokana na mafuriko yaliyotokea nchini Malawi. Kuna zaidi ya watu 200,
000 hawana makazi na kwamba, makazi ya watu, shule na miundo mbinu imeharibiwa sana.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.