Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linapenda kuwapongeza wanasiasa na wananchi wote
ambao hadi wakati huu wameendesha kampeni zao kwa kuzingatia misingi ya haki, amani
na utulivu na kwamba, wanapaswa kuendelea katika mwelekeo huu, ili kweli cheche za
matumaini ya amani na utulivu ziweze kurejea tena nchini humo, ambako kuna watu wanateseka
kutoka na mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na Kikundi cha Boko Haram.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Nigeria limeyasema haya katika mkutano wake wa mwanzo wa Mwaka,
uliofanyika hivi karubuni mjini Ibadan. Wanasikitika kusema kwamba, kuna baadhi ya
wanasiasa wanaoendesha kampeni zao kwa kupandikiza chuki na uhasama kati ya watu,
ili kutafuta kura kwa nguvu, jambo ambalo ni hatari kwa umoja na mshikamano wa kitaifa.
Maaskofu
Nigeria wanaitaka Serikali kuhakikisha kwamba, inalivalia njuga tatizo la Boko Haram
ambalo kwa sasa ni tishio la kimataifa na chanzo cha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.
Maaskofu wanasema, Kanisa kwa upande wake, litaendelea kutangaza Injili ya Uhai, tangu
pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika
kadiri ya mpango wa Mungu. Maaskofu wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi
mema nchini Nigeria kusimama kidete kupinga utamaduni wa kifo, udini, ukabila na umajimbo.
Wazazi wawajibike kikamilifu katika maisha ya ndoa na familia.
Na Padre Richard
A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.