2015-01-24 09:21:24

Miaka 50 si haba!


Kuna umati mkubwa wa watu wanaotaka kumfahamu Mwenyezi Mungu, changamoto kwa viongozi wa Kanisa nchini Vietnam kuanzisha mikakati makini ya shughuli za kichungaji, ili kuweza kuzima kiu ya Watu wa Mungu nchini humo sanjari na kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji mpya. Jimbo la Da Nang, tarehe 18 Januari 1963, liliundwa rasmi na Mtakatifu Yohane XXIII, wakati wa maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kumbe, tayari miaka hamsini imekwisha yoyoma!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Ijumaa tarehe 23 Januari 2015 na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu katika hija yake ya kichungaji nchini Vietnam. Anasema, Kanisa pia linaadhimisha Jubilee ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka wa kichungaji wa kazi za kimissionari za Kanisa, maarufu kama "Ad Gentes", unaokazia dhamana ya uinjilishaji na majiundo makini miongoni mwa vijana.

Kardinali Filoni anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya imani nchini Vietnam kwa kipindi cha miaka mia nne iliyopita, changamoto kwa Familia ya Mungu, kuendelea kuwa aminifu kwa imani na Mapokeo ya Mama Kanisa; kwa kujikita katika ushuhuda wenye mguso na mashiko. Katika Ibada ya Jubilee ya miaka 50 ya Jimbo Katoliki la Da Nang, Kardinali Filoni ametoa Sakramenti ya Ubatizo kwa Wakatekumeni 50 na watoto 10; wote hawa wamepewa salam na baraka tele kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Waamini wanakumbushwa kwamba, hizi ni juhudi za Mwenyezi Mungu ambaye kwanza kabisa amewatafuta, ili kuwakirimia zawadi ya imani, ambayo wanapaswa pia kuwashirikisha jirani zao kwa njia ya ushuhuda, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Yesu katika maisha na utume wao. Yesu huyu lazima aabudiwe moyoni na kukiriwa katika vinywa na uhalisia wa maisha binafsi na yale ya hadhara.

Ikumbukwe kwamba, imani ni jambo la Jumuiya linalowaunganisha watu kwa pamoja na hivyo kujenga Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Waamini wanapaswa kuwa ni kielelezo makini cha Fumbo la Utatu Mtakatifu, umoja na mshikamano ulioneshwa na Mitume waliokuwa wamemzunguka Yesu, huku wakiongozwa na Roho Mtakatifu. Familia ya Mungu nchini Vietnam inatumwa kuwatangazia watu Injili ya Furaha kwa kujikita katika ari na moyo wa kimissionari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.