2015-01-23 09:58:16

Je, uko tayari?


Neno utume linaendana na ufuasi. Kwa maana nyingine, mtume ni mfuasi. Leo tena neno/swala la utume linawekwa mbele yetu. Yaweza kuonekana kuwa nabii Yona hakuwa na bahati katika maisha yake ya utume kama ionekanavyo katika somo la kwanza. Lakini inaonekana wazi kuwa, Mungu ana mpango nasi na akituhitaji, ni lazima atatupata.


Licha ya hali yetu ya awali, akitupata, aliyeitwa anakuwa mshindi dhidi ya ulimwengu. Neno la Mungu katika – 1 Yn. 5:4-5 – latutafakarisha sana katika hili - kwa maana yote yaliyo na asili yake katika Mungu huushinda ulimwengu. Na ushindi ushindao ulimwengu ndiyo imani yetu. Ni nani awezaye kuushinda ulimwengu isipokuwa yeye tu asadikiye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu? Yona alipoitwa hakuijua nguvu hii ya Mungu. Alidhani angeweza kuamua mwenyewe, hata kupingana na wito wa Mungu.


Mtakatifu Agustino wa Hippo anaandika wazi – tumeumbwa kwa mapenzi yake Mungu ila kupata wokovu ni juhudi binafsi. Maana yake ni kuwa, kila mmoja wetu anapaswa kushiriki kikamilifu katika mpango wa Mungu wa ukombozi.
Mwanamuziki maarufu – mwitaliano – Paganini – alipiga muziki kwa miaka mingi. Siku moja baada ya kupiga muziki, wakati wa mapumziko akagundua kuwa hakutumia gitaa lake ambalo hutumia kila siku na kumpatia umaarufu. Akaghadhabika sana, kiasi cha kutokuwa tayari kuendelea na kipindi cha pili. Msaidizi wake alitumia nguvu ya ziada kumshawishi kuwa muziki umepigwa kama kawaida na watu wamefurahi mno.


Basi kwa moyo mzito akarudi kuendelea kutumbuiza. Ila huku akiendelea kutumbuiza, alikuwa akishangaa jinsi watu walivyokuwa wanamshangilia na kufurahi. Ni toka hapo alipogundua kuwa muziki wa kweli hutoka moyoni. Chombo cha muziki ni zana inayosaidia tu. Muziki wa kweli hutoka moyoni.


Tunaona katika somo la kwanza - Yona anaitwa na kutumwa kwa watu wa Ninawi ili kuongea neno la toba. Ninawi ulikuwa mji mkuu wa Assyria. Yeye hakuwa tayari kufanya hilo. Ikumbukwe kuwa Assyria ilikuwa adui mkubwa wa taifa la Israeli. Kwa mtindo wao wa maisha na uadui wao na taifa la Israeli aliamini fika kuwa wasingekuwa tayari kusikia sauti ya nabii. Aliamini kuwa hana haja ya kupoteza muda wake. Hivyo anatoroka wito wa Mungu. Kilichotokea tumesikia katika somo la kwanza. Mambo yanakuwa kinyume na anajikuta Ninawi. La kushangaza ni kuwa baada ya neno la unabii, neno la toba – watu wote wanakuwa tayari kuongoka.
Katika somo hili – twaona ushindi wa Mungu dhidi ya maovu. Kwa somo hili tunapata tangazo la toba la wenye dhambi. Yona anakuwa chombo cha Mungu katika kutangaza haja hiyo ya toba.


Katika somo la Injili – twaona utume wa kwanza wa hadhara wa Yesu huko Galilaya na tangazo la uwepo wa ufalme wa Mungu. Sawa na somo la kwanza, lipo tamko la toba na imani. Katika geuko hilo, upo wito wa wafuasi wa kwanza wa Yesu. Licha ya hali yao ya kawaida, Yesu anawachagua. Ni muhimu sana hapa. Wanaacha mtindo wao wa maisha, wanakuwa wafuasi.


Somo la pili – linatupatia mwelekeo wa kile tunachotakiwa kuwa. Tutumie yote tuliyonayo na vizuri ili kumpata Kristo. Yona alionekana katika hali yake. Akaitwa na kutumwa na Mungu kama alivyokuwa. Wafuasi wa kwanza walionekana katika hali yao. Yesu akawaita. Wakaacha yote wakamfuata. Huu ndio utume au ufuasi wa kweli.


Tujaribu kuangalia nafasi yetu leo katika utume au ufuasi kama tulivyoitwa na Mungu. Tukumbuke kuwa kwa ubatizo wetu sisi sote tumeitwa kuwa mitume au wafuasi wake Bwana. Sisi sote ni wamisionari. Tutafakari katika baadhi ya changamoto zilizo mbele yetu na kuona namna ambavyo tunaitwa kutumikia;
Woga ulipo katika kila mmoja wetu wa kufanya badiliko la hali ya maisha, msimamo au mitizamo binafsi sisi tunapanga, Mungu anapangua. Tumeona jinsi Mungu anavyoita na kutuma Yona, kina Petro. Mara ngapi tumepinga mpango wa Mungu? Wengi wetu tunaliita sana jina la Mungu na tunampenda sana Mungu. Lakini tukitakiwa kufanya kazi maalumu ya Mungu, tunasita sana na hata kukataa.


Tuangalie wengi wetu tunavyokwepa uongozi katika ngazi mbalimbali za kanisa kama uongozi katika ngazi ya walei. Bado kina Yona wengi wapo kati yetu.
Ni kwa kiasi gani tunahitajika au tumehitajika na hasa pale penye shida lakini hatukufanya au hatukuwa tayari kwenda au tumekwenda kwa shingo upande? Mara ngapi tumetupia kisogo matatizo ya wengine ambapo yalihitaji waziwazi msaada wetu? Inapotokea padre au mmisionari anakataa kwenda kufanya utume sehemu au maeneo fulani kwa sababu ni sehemu maskini au watu ni maskini au pengine tunasema wale watu ni wagumu.


Ninawi yetu ni wapi au kitu gani leo? – mahali gani au kitu gani katika mazingira yetu ya leo? Kwa Wayahudi wa karne ya kwanza – Ninawi ulikuwa ni mji usiomjali Mungu, umejaa dhambi na dhuluma. Ulifanya madhara makubwa kwa taifa la Israeli, ikiwa hata kuharibu hekalu la Yerusalemu. Hawakuwa na hofu ya Mungu. Hivyo kwa mcha Mungu kama Yona na Myahudi, Ninawi ulikuwa mbali na neno la Mungu. Dhambi ilitawala na nia ya kubadilika haikuwepo. Hivyo kwenda Ninawi ilikuwa ni kupoteza muda.


Baba Mtakatifu leo katika fundisho lake anaalika Kanisa na Wakristo kutoka katika mazoea yao na kupeleka habari njema pembezoni au pasipo na matumaini – angalia Injili ya Furaha. Angalia alichofanya Yona pale Ninawi. Watu walisikia neno na wakafanya toba. Unaonaje ndugu yangu kama leo ukiamua kufanya kitu ili kuokoa hali isiyoridhisha katika mazingira yetu kiimani, kimaadili, kiuchumi, kisiasa na kijamii?

Tumsifu Yesu Kristo,

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.