2015-01-23 11:22:04

Familia haina mbadala, piga ua galagaza!


Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na umuhimu wake katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii kwa ujumla ni kati ya mada kuu zilizofanyiwa kazi na Baraza la Maaskofu Katoliki Gabon, katika mkutano wake wa mwaka uliohitimishwa hivi karibuni mjini Libreville. Huu ni mwendelezo wa tafakari ya kina kutoka kwa Familia ya Mungu nchini Gabon, kama sehemu ya maandalizi ya maadhimiso ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia, itakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015.

Maaskofu wanasema, familia ni urithi mkubwa wa binadamu na kwamba, inachukua nafasi ya kwanza katika maisha, uzoefu na mang'amuzi ya kibinadamu. Hapa kuna haja ya kutambua na kuheshimu haki msingi za wanawake na watoto pamoja na kukuza utamaduni wa majadiliano kati ya wanandoa pamoja na kuwasaidia vijana kufanya maamuzi magumu ya kufunga ndoa na kuachana na tabia ya uchumba sugu, mtindo wa maisha ambao kwa sasa umepitwa na wakati!

Vijana wakipendana waoneshe mapendo yao ya dhati mbele ya Kanisa, ili kushiriki kikamilifu katika kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Familia, katika ukweli na uwazi, tayari kushiriki kikamilifu katika malezi na makuzi ya watoto wao: kiroho na kimwili.

Baraza la Maaskofu Katoliki Gabon, linasikitika kusema kwamba, leo hii, familia nyingi zinakabiliwa na matatizo, changamoto na fursa ambazo zinawapelekea kumezwa na malimwengu, kiasi hata cha kukengeuka na kusahau tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, maadili na utu wema. Bila familia, jamii itajichumia majanga makubwa kwa siku za usoni na kwamba, itayumba na kwamba, binadamu atayumba na kuyumbishwa kama "daladala" iliyokatika usukani.

Kinzani dhidi ya familia ni kinzani zinazolenga kudhohofisha msingi wa familia unaojikita katika upendo kamili kati ya bwana na bibi; upendo na mshikamano ambao haupaswi kutenguliwa hadi pale kifo kitakapowatenganisha. Utamaduni wa kifo unaojichimbia katika sera za utoaji mimba, kifo laini na mauaji ni mambo ambayo ni hatari sana kwa maisha ya ndoa na familia, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutangaza Injili ya Uhai inayojikita katika Familia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Gabon linasema, kuna haja kwa viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanatoa majiundo makini kuhusu maisha ya ndoa na familia pamoja na kuwasaidia wanandoa watarajiwa na vijana kukabiliana kikamilifu na changamoto za maisha ya unyumba. Wanandoa wajiandae kikamilifu: kiroho na kimwili; kimaadili na kiuchumi, ili kufurahia maisha ya ndoa na familia. Maaskofu wanaitaka Serikali kujikita katika utawala wa haki na sheria; kwa kupinga rushwa na ufisadi kwa nguvu zote kwani mambo haya pia ni hatari kwa maisha ya unyumba.

Baraza la Maaskofu Katoliki Gabon linawataka waamini na wananchi wote wa Gabon katika ujumla wao kuhakikisha kwamba, wanajikita katika kulinda, kutunza na kudumisha misingi ya haki na amani, wakiwajibika kwa Mungu na jirani zao.

Ikumbukwe kwamba, amani ni zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu na kwamba, mchakato wake daima ni endelevu, changamoto ya kuheshimu, kulinda na kudumisha utu wa mwanadamu. Wananchi wajenge utamaduni wa upendo, udugu na mshikamano wa kitaifa; mambo msingi katika ukuzaji wa haki na amani. Amani duniani inachipuka kutoka katika upendo kwa Mungu na jirani, ndiyo maana watu wote wanahamasishwa kueshimiana na kupendana kama Watoto wateule wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.