Bikira Maria linda kazi na matunda ya Uinjilishaji!
Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu,
Alhamisi, tarehe 22 Januari 2015 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Madhabahu
ya Bikira Maria Mama wa Mungu wa La Vang, nchini Vietnam, kwa kumwomba Bikira Maria
kulinda kazi na matunda ya mchakato wa Uinjilishaji sehemu mbali mbali za dunia.
Bikira
Maria ni Mama wa Neno wa Mungu, Injili Hai, aliyethubutu kumsindikiza Mwanaye Mpendwa,
Yesu Kristo katika hija ya maisha yake hapa duniani na wakati wa Pentekoste, akashuhudia
Kanisa likizaliwa na kuanza kuenea sehemu mbali mbali za dunia, leo hii Injili imefika
hata Vietnam.
Kardinali Filoni anasema, Bikira Maria ni Mama mwenye ujasiri,
aliyediriki kusimama chini ya Msalaba, akakubali kupokea dhamana ya kuwa ni Mama wa
wote, tangu wakati ule. Bikira Maria ameendelea kuwa kweli ni Mama wa wote, kielelezo
kwamba, Yesu alipenda kuwazawaidia wafuasi wake Bikira Maria, ili aweze kuwa kweli
ni msaada na mwombezi katika hija ya maisha yao. Bikira Maria anaendelea kuwa ni kielelezo
cha uwepo wake endelevu katika Madhabahu mbali mbali duniani, kama vile: Lourdes,
Fatima na La Vang, nchini Vietnam.
Hapa palikuwa ni kimbilio la waamini walipokumbana
na madhulumu na nyanyaso za kidini, wakapata ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ndiyo
maana haya ni Madhabahu ya kitaifa, mahali pa kukutana, kusali, kutafakari na kuomba
ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Kardinali Fernando Filoni, kwa niaba ya Familia ya
Mungu nchini Vietnam, amemshukuru Yesu Kristo kwa kuwazawadia zawadi ya Bikira Maria
na kwamba, anamwomba aendelee kusaidia mchakato wa Uinjilishaji mpya Barani Asia.