2015-01-22 08:25:02

Watoto wanateseka sana kwenye maeneo ya vita!


Shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, katika taarifa yake linasema kwamba, kutokana na vita pamoja na machafuko ya kijamii yanayoendelea huko Nigeria, kuna zaidi ya watu millioni moja wanaokimbia ili kusalimisha maisha yao na kwamba, kuna watoto wanaopoteza maisha na nafasi za masomo kutokana na kuhofia usalama wa maisha yao.

Bwana Manuel Fontaine, mkurugenzi mkazi wa UNICEF kanda ya Afrika anasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete ili kuzuia mashambulizi na vita inayoendelea kuenea katika nchi mbali mbali zilizoko Kaskazini mwa Afrika; hasa Chad, Cameroon na Niger; nchi ambazo kwa sasa zinaanza kugeuzwa kuwa ni uwanja wa vita.

UNICEF inaendelea kushikirikiana na wadau mbali mbali ili kuhakikisha kwamba, watoto wanaokimbia vita na kinzani za kijamii wanahudumiwa vyema, kwa kupatia huduma msingi, sanjari na kuwapatia chanjo dhidi ya magonjwa mbali mbali.







All the contents on this site are copyrighted ©.