2015-01-22 09:38:09

Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia!


Baraza la Maaskofu Katoliki Uswiss, linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia, itakayoadhimishwa mjini Vatican mwezi Oktoba 2015, kwa kusali na kuchangia hoja, mintarafu maswali dodoso yaliyotolewa na Sekretarieti ya Sinodi za Maaskofu.

Majibu ya maswali haya ni muhimu ili kuiwezesha Sekretarieti kutunga hati ya kutendea kazi, ijulikanayo kama "Instrumentum Laboris". Majibu ya maswali dodoso yanapaswa kuwa yamekwishawasilishwa mjini Vatican ifikapo tarehe 15 Aprili 2015. Maaskofu wanasema, maoni, hoja na tafakari zinazotolewa na Familia ya Mungu nchini Uswiss zioneshe mang'amuzi ya maisha ya kiroho yanayogusa: matatizo, changamoto na fursa zilizopo, ili kweli Kanisa liendelee kutangaza Injili ya Familia, katika ulimwengu unaoendelea kukengeuka katika misingi ya maadili na utu wema.

Maaskofu wanawahamasisha waamini kufanya majadiliano ya kweli, kama sehemu ya ushiriki wao katika hija ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia. Wanafamilia walioguswa na kutikiswa katika matatizo na changamoto hizi, washirikishe mawazo na maoni yao, ili Kanisa liweze kuyatambua na hatimaye, kuyapatia majibu muafaka kwa wakati wake.

Maaskofu wanawahamasisha waamini kuandaa matukio mbali mbali katika kipindi cha mwaka huu, ili kujadili, kukuza na kuendeleza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kuonesha ushiriki mkamilifu na maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, itakayoadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015, kwa kuongozwa na kauli mbiu "Wito na utume wa Familia ndani ya Kanisa na Ulimwengu mamboleo".

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.