2015-01-22 11:56:37

Njia mbadala ya kupambana na baa la umaskini!


Chuo kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki na Kati, CUEA kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Vyuo vikuu vya Kikatoliki, IFCU, limechapisha kitabu kinachobainisha njia mbadala ya kupambana na baa la umaskini, matunda ya utafiti uliofanywa kwa kipindi cha miaka miwili, yaani kuanzia mwaka 2011 hadi mwaka 2012.

Utafiti huu umepembua kwa kina na mapana mikakati, sera na programu za kupambana na baa la umaskini mintarafu Serikali; mikopo nafuu inayotolewa kwa wajasiriamali pamoja na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa kwa kujikita katika mshikamano na maendeleo ya watu kwa kusaidiana katika umoja na upendo.

Utafiti huu unabainisha kwamba, ili kweli umaskini uweze kupewa kisogo kwa wananchi wengi Barani Afrika kuna haja ya kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo: sera na mipango thabiti inayoratibiwa na kutekelezwa na wadau mbali mbali na kwamba, mikakati ya kichungaji inayotolewa na Mama Kanisa inaweza pia kuwa ni njia mbadala ya kupambana na baa la umaskini, linaloendelea kusababisha majanga mengi Barani Afrika.

Huu ni mchango uliotolewa na Askofu mkuu Zacchaeus Okoth, Mwenyekiti wa Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, wakati wa kuzindua kitabu hiki. Askofu mkuu Okoth ameishauri Serikali ya Kenya kuangalia tena sera, mikakati na programu ya marekebisho ya uchumi sanjari na mapambano dhidi ya baa la umaskini nchini humo. Huduma zinazotolewa kwa njia ya mshikamano zimesaidia hata watoto wa maskini kuendelea na masomo pamoja na kupata huduma msingi, kiasi cha kusaidia katika mchakato wa maboresho ya maisha ya watu wengi hasa vijijini.

Ili kupambana na umaskini wa hali na kipato, watafiti kutoka CUEA wanasema, kuna haja kwanza kabisa kuhakikisha kwamba, mambo yote yanayosababisha na kupelekea kukua na kuongezeka kwa umaskini wa hali na kipato yanashughulikiwa kikamilifu na kwamba, mshikamano wa upendo unaoongozwa na kanuni ya auni katika utekelezaji wa mikakati ya shughuli za kichungaji inayofanywa na Mama Kanisa ni njia muafaka ya kupambana na baa la umaskini duniani.

Hapa kuna haja ya kushirikishana tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili na kwamba, haitoshi kushirikishana rasilimali vitu na fedha tu! Ukweli, uwazi na maendeleo na mafao ya wengi ni mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika mapambano dhidi ya baa la umaskini. Wananchi wajenge utamaduni wa kushirikishana baraka na tunu msingi za maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Kwa msaada wa CISA, Nairobi, Kenya.







All the contents on this site are copyrighted ©.