Kardinali Laurenti Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC amekemea
sana mauaji ya watu wasiokuwa na hatia yaliyofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama
katika harakati za kusimamisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba unaotaka kutoa mwanya
kwa Rais Joseph Kabila, ambaye amekuwepo madarakani kuanzia mwaka 2001 kuendelea kukaa
madarakani. Kardinali Monsengwo anasema, si haki kwa vikosi vya ulinzi na usalama
kuua raia ambao, wanapaswa kuwalinda na kuwatetea.
DRC kunawaka moto kwa wananchi
kuonesha nguvu ya umma ili kupinga mchakato wa kutaka kupindisha Katiba, ili kutoa
mwanya kwa Rais Joseph Kabila kuendelea kuwa madarakani. Wananchi katika patashika
nguo kuchanika, wanaendelea kukumbana na rungu la dola.
Baraza la Maaskofu
Katoliki DRC linapinga mchakato wa kutaka kupindisha Katiba ya nchi kwa ajili ya mafao
ya watu wachache ndani ya jamii na kwamba, wananchi nao wanapaswa kutumia njia za
kidemokrasia na amani, ili kuhakikisha kwamba, utawala wa sheria unalindwa na kuzingatia,
vinginevyo, DRC itaendelea kuwa ni uwanja wa fujo, mwenye nguvu mpishe! Jumuiya ya
Kimataifa inaitaka Serikali ya DRC kuheshimu Katiba.