2015-01-22 08:58:13

Changamoto za kichungaji!


Baraza la Maaskofu Katoliki Korea mara baada ya hija ya kitume iliyofanywa na Baba Mtakatifu Francisko nchini humo mwaka 2014, limefanya utafiti wa kina ili kufahamua vipaumbele na matarajio ya Familia ya Mungu nchini Korea ya Kusini, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa mikakati ya Uinjilishaji mpya!

Familia ya Mungu nchini Korea, inapenda kuona Kanisa ambalo ni maskini kwa ajili ya maskini; Kanisa ambalo linauwezo wa kuishi na kushuhudia Injili ya Furaha; daima likijita katika kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Haya ndiyo mambo makuu ambayo Familia ya Mungu Korea ya Kusini, inatarajia kuyaona yakifanyiwa kazi na Mama Kanisa katika maisha na utume wake nchini humo.

Wachunguzi wa masuala ya maisha na utume wa Kanisa wanasema kwamba, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Korea ya Kusini, imeacha chapa ya kudumu katika akili na mioyo ya wananchi wa Korea na kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki linataka kufanyia kazi cheche za uwepo wa Baba Mtakatifu nchini Korea ya Kusini kama kikolezo cha utekelezaji wa mikakati yake ya shughuli za kichungaji, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu, Korea ya Kusini.

Maaskofu Katoliki Korea ya Kusini bado wanakumbuka changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu katika maisha na utume wao, ili kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni walinzi wa kumbu kumbu hai na matumaini miongoni mwa Familia ya Mungu na kwamba, wanapaswa kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kanisa halina budi kuguswa na shida na mahangaiko ya watu, ili kuwahudumia kwa imani, matumaini na mapendo makubwa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Korea ya Kusini katika maswali dodoso waliyoulizwa kwa waamini, wanasema kwamba, waamini wangelipenda kuwaona viongozi wa Kanisa wakijihusisha zaidi na zaidi katika mchakato wa majadiliano yanayopania pamoja na mambo mengine kukuza na kudumisha haki jamii; Wakleri waoneshe unyenyekevu badala ya kutumia "rungu" katika utekelezaji wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Watawa kwa upande wao, waendelee kuonesha ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika huduma makini kwa Familia ya Mungu, nchini Korea ya Kusini.

Waamini walei, waachane na tabia na mambo yanayowagawa na kuwasambaratisha na badala yake, wajikite katika maisha ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na matendo ya huruma kama kielelezo cha imani tendaji. Waamini wanasema, ikiwa kama kweli Kanisa Katoliki nchini humo linataka kujipyaisha na kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji mpya kwa ari na moyo mkuu, halina budi kujenga mazingira ya upendo na ukarimu, utakaoliwezesha Kanisa kuwa ni mahali penye mvuto wa maisha ya kiroho kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Matokeo ya utafiti huu yametolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Korea ya Kusini katika mkutano wake wa mwanzo wa mwaka uliofanyika hivi karibuni huko mjini Seoul.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.









All the contents on this site are copyrighted ©.