2015-01-21 10:57:41

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican kipindi Tafakari Neno la Mungu, leo tunaangalia maisha yetu tukiongozwa na Neno la Mungu lililo chimbuko ya furaha yetu. Ni Dominika ya tatu ya mwaka wa Kanisa. Ujumbe tunaopaswa kuubeba mioyoni mwetu ni Toba na kuitikia wito utokao kwa Mungu. RealAudioMP3

Katika somo la kwanza tunamwona Nabii Yona anaitwa na Mungu ili kutangaza habari ya toba kwa mataifa. Yona anajitahidi kukwepa mwaliko wa Mungu lakini Mungu aliye mwaminifu katika uamuzi wake hakati tamaa mpaka Yona atakapokubali mwaliko wake. Baada ya kukubali mwaliko wa Mungu nabii Yona anakwenda Ninawi kutangaza ujumbe wa Mungu unaowaalika watu kutubu katika kipindi cha siku arobaini vinginevyo anaangamiza mji huo.

Basi watu wa Ninawi wakijua upendo wa Mungu na hukumu zake kuwa ni za haki wanaitika wito wa toba, wanajivika mavazi ya magunia, alama ya toba na wanabadilisha maisha yao. Kwa sababu Mungu hubaki mwaminifu katika ahadi zake anaghairi angamizo ambalo angelitenda kwa Ninawi.

Mpendwa, yako mambo mengi ya kujifunza katika hili kwanza wakati fulani inatokea katika maisha yetu tunakataa wito wa Mungu wa toba na hata wa kwenda kutangaza habari njema. Kumbe yafaa kuangalia kwa makini ili tusije tukapoteza nafasi ya wokovu kwa sababu ya kukataa mwaliko wa toba na wito wa kimisionari. Kumbukeni Kanisa letu kwa asili ni la kimisionari. Twajifunza kuwa bidii kidogo tu katika kubadilisha mwenendo wetu mbaya yamfanya Mungu aghairi nia yake.

Mtume Paulo anapowaandikia Wakorinto yuko katika mtindo uleule wa kuweka maisha yetu mikononi mwa Mungu. Kuitika daima upendo wa Mungu na hivi kutumia mali ya dunia kama chombo cha kutusaidia kujenga mahusiano mazuri na Mungu mwenyezi. Anawaambia kuwa muda tulionao hapa duniani ni mfupi na hivi tuutumie vema kwa ajili ya toba na hivi kuambatana na mapenzi ya Mungu.

Wazo la toba na wito linajitokeza waziwazi katika Injili ya Marko. Toba ni mwanzo wa Injili ya Marko pale tunaposikia tubuni na kuiamini Injili (Mk 1:15) Bwana anataka watu watubu ili watoe nafasi mioyoni mwao kwa ajili ya upendo wa Mungu. Bila toba na kuamini, mmoja hawezi kupokea habari njema. Ndiyo maana Kanisa husisitiza waamini wapokee daima sakramenti ya kitubio njia ya neema za Mungu.

Sehemu ya pili ya Injili ya dominika hii ni juu ya ni wito wa Mitume. Bwana anawaita mitume wamfuate na wafanye kazi ya toba na wasaidie kazi ya wokovu. Katika kuwaita yapo mambo ambayo yafaa kuyaangalia. Kwanza wito ni zawadi na pili ndani ya wito kuna Msalaba.

Tunamwona Bwana akiwaita Mitume wakati huohuo yuko kazini, yuko njiani, hasimami na kuanza kuwabembeleza bali anasonga mbele, kwa maana hiyo nasi hatukuitwa ili kubembelezwa bali kushika njia ya Bwana inayoambatana na umisionari, wajibu na mateso ndani yake. Ndiyo kusema, kumfuasa Bwana si kwenda likizo bali kukaza moyo na kuishi mapenzi ya Mungu. Wanaoitwa wanaacha kila kitu pamoja na wazazi wanaanza safari ya wokovu. Wanaitika wito kama watu wa Ninawi ambao mara moja wameitika na kubadili maisha yao.

Mpendwa unayenisikiliza yakupasa kujenga utamaduni wa toba ili kwa njia hiyo basi ukomavu wa wito uliokabidhiwa siku ya ubatizo wako utakuwa siku kwa siku ukiongezeka.

Ninakutakieni heri na baraka za Mungu katika kushika na kutenda mapenzi ya Mungu ambapo watakiwa kwanza kutubu na kisha kuanza safari bila kuwazawaza mambo ya jana au ya kidunia bali yaliyo ya kimungu.

Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.