Tangazo maalum: “Muda umefika na wakati ni huu wa kufanya mapinduzi na kuingiza utawala
mpya!” Ninaposema muda au wakati simaanishi muda wa saa ya mkononi ambayo wagiriki
wanaita kronos, la hasha, bali ni muda ambao wanaita kairos, yaani wakati mwafaka,
wakati utakiwao. Muda mwafaka wa kufanya mapinduzi ndiyo huu, ukikosa kufanya mageuzi
sasa basi “itakula kwako.” Mapinduzi hayo ni ya serikali, ya siasa, ya dini, ya kiroho,
ya kimaadili kwa ulimwengu mzima. Utekelezaji wa tangazo hilo mtaushuhudia.
Hebu
nikudokezee kwa kifupi mazingira yalivyoandaliwa ya mapinduzi hayo. Leo utashuhudia
jinsi vituko vilivyojipangana pamoja katika mchakato huo wa mapinduzi. Mosi, tutamshuhudia
bwana mmoja aliyekuwa amemnadisha na kumtangaza sana huyo mleta mapinduzi ametiwa
gerezani, pili, Mwanamapinduzi mwenyewe utamwona anatembea kwa uhuru wote huku na
huku barabarani akitafuta wafuasi, anatembelea ufuoni mwa ziwa, anaona mashua, anaona
nyavu na wavuvi na anawaita kumfuata, nao wanatelekeza nyavu na baba zao wanainuka
kumfuata. Hii ndiyo kasi mpya anayoanza nayo, yaani kupita kujinadisha na kutangaza
adhima yake ya mapinduzi anayotaka kuyafanya ya kutaka kuingiza utawala mpya.
Tuanze kuviona vituko hivyo kimoja baada ya kingine: “Baada ya Yohane kutiwa gerezani,
Yesu akaenda Galilea kufundisha.” Maana yake, hata kama Yohane aliyembatiza na kumtangaza
Yesu amenyamazishwa kwa kutiwa gerezani, Neno jipya linachukua kasi yake mara moja.
Yesu, anazunguka vijijini kuanza kampeni zake. Haanzi kazi mjini Yerusalemu, kwenye
hekalu kubwa na makuhani wakuu, na wakuu wa serikali na siasa, bali anaanza kijijini
huko Galilea ya upagani, kwa watu mchanganyiko waliodharauliwa tena katika Sinagogi
au kigangoni.
Huko anaanza kutoa tangazo la mapinduzi: “Wakati umetimia,
Utawala wa Mungu umekaribia; Ongokeni na kuamini Injili,” ni wakati mwafaka wa kufanya
mapinduzi kwa maisha mazima ya binadamu. Maana yake, wale waliojulikana kuwa watu
wa maana hapa duniani kutokana na utajiri wao, basi sasa ndiyo mwisho wa habari. Wale
wenye kuheshimika kutokana na utajiri sasa watakuwa maskini. Wakuu wanashushwa na
wanyonge wanapandishwa. Hayo ni mapinduzi ya kweli kwani watu wanarudishiwa thamani
ya utu wao.
Halafu “Utawala wa Mungu umekaribia” hayo ni maneno ya kimapinduzi
yaonekana kama yanashuka kutoka mbinguni hadi duniani, toka kwa Mungu hadi kwa binadamu,
yaani ufalme huu unatoka mbinguni, Mungu anajitokeza kama binadamu. Mungu anataka
binadamu awe binadamu inavyotakiwa kuwa siyo mnyama. Kumbe maneno “Ongokeni na kuamini
Injili” yanaonesha kupanda toka binadamu kwenda juu mbinguni, yaani ni wajibu wa
binadamu kwa Mungu. Njia pekee ya kuongoka na kuwa binadamu ni “kuamini Injili” Yesu
anasema: ongokeni, aminini, sadikini habari njema, msidanganyike na mambo mengine
na watu wengine. “Aminini ninachosema mimi.” Yohane mbatizaji na manabii walionya
kuwa, kama hamwongoki mtaadhibiwa. Lakini Yesu anataka kuongoka kule kwa kubadili
fikra.
Mungu aliyejulikana kuwa anahifadhi wenye nguvu na ni mkali, mlipiza
kisasi, hali iliyowakuza kichwa wafalme na watawala hao sasa ni tofauti yabidi kubadili
fikra. Ama kweli Yesu ni mwana mapinduzi. Baadaye kidogo mtaona jinsi Yesu atakapoyafanya
mapinduzi yenyewe pale atakapoponya, atakapotakasa, atakapofungua vizingiti vya milango,
atakapopatanisha watu na wale waliotengwa na jamii.
Baada ya tangazo hilo
la mapinduzi anapita kuchagua wafuasi wa kufanya naye kazi hiyo ya mapinduzi. Wafuasi
hao hawachaguliwi kutoka katika mazingira ya kanisa, au mazingira ya kusali, bali
ameamua kuwachagua katika mazingira ya ziwani, watu wakiwa katika kazi zao za kawaida
za uvuvi, inamaanisha kwamba ufalme wa Mungu unaingia katika maisha ya watu wa kawaida.
Huko ziwani katika tembeatembea yake anamwona Simoni. Mara moja anafikiri
kwamba huyu anaweza kuwa tofali la kwanza la ujenzi. Halafu anamwona Yohane na anagundua
kuwa huyo ataweza kuwa na lugha ya kufaa kutangaza upendo. Baadaye zaidi anamwona
hata malaya ambaye anaweza kupenda vizuri kuliko anavyofanya hadi sasa. Huo ndiyo
mwono wake wa uumbaji mpya.
Kumbe, Bwana anaweza kuniona hata mimi labda
nitaweza kushirikiana naye hapa ulimwenguni kwa kutumia mikono yangu kichwa changu
na moyo wangu. Kisha anawaambia aliowaiga: “Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi
wa watu.” Kinyume cha mategemeo yao na yetu. Watu hawa walidhani mwito huu ni wa kupata
cheo au kudokezewa kufanya kazi yenye kipato zaidi au kazi yao inaboreshwa, labda
watafanya kazi ya utafutaji lulu au hazina ya thamani. Kumbe wanaambiwa zoezi la uvuvi
linaendelea lakini sasa mtazamia ulimwenguni kote na kuvua watu.
Watu
ndiyo wanaokuwa lulu na hazina, maana yake itawabidi kufanya juu chini kuwatafuta
watu popote pale hao watu wanapojidhani wamefika kumbe hawajafika, pale wanapoona
wamepata kumbe wamepatikana, au wanapoona wamestarehe na kuvuta hewa safi kumbe wamekaa
karibu na shimo la choo wakivuta hewa chafu. Wafuasi yabidi waende wakawavue watu
toka katika mazingira hayo ya ovyo na kuwaweka safi. Kwa hiyo Yesu amewaonesha wafuasi
wake miondoko miwili ya kufuata. Mosi kufuata mgongoni pake na pili kuwaendea watu
na kuwafundisha.
“Mara wakaziacha nyavu zao na kumfuata.” Wavuvi wanafahamu
kazi ya nyavu ni kunasa samaki na kuwavua toka majini walimo huru. Samaki akinasa
nyavuni hawezi kutoka kirahisi. Tukijiangalia kwa makini hata sisi wakati fulani tunajinasa
na kukamatika katika nyavu mbalimbali za maisha. Tunavirigwa vibaya hata tunashindwa
kujinasua. Wengine tunanaswa kwenye nyavu za ulevi, wengine kwenye ngono, wengine
kwenye madaraka, wengine kwenye wivu, wongo, maraharaha, uvivu, hasira, pesa, utajiri
nk. Huko tulikonaswa ndiko tunajisikia tumefika na hatutaki kutoka. Je, mwenzangu
umenaswa kwenye nyavu zipi?
Huo ndiyo ukisikia ulimwengu wa kupagawa na
pepo mchafu tutakayemsikia dominika ijayo. Aina nyingine ya nyavu zilizotuviriga na
tunazopaswa kujinasua nazo ndizo zile tunazosikia pale wanapoitwa waana wa Zebedeo.
Yasemwa, kwamba walipoitwa, “Wakamwacha baba yao mashuani pamoja na nyavu wakamfuata.”
“Baba” yamaanisha mapokeo, na “Nyavu” ni desturi. Watoto hawa maram moja wakaachana
na mambo ya kale waliyozoea, wakaachana na thamani za kale zinazopingana na mambo
mapya. Nasi tuzikate nyavu zilizotunasa na tumfuate mwalimu huyu mwana mapinduzi na
mwanakondoo katika safari yake. Wakati ni huu wa kufanya mapinduzi!