2015-01-21 08:20:09

Cheche za matumaini mapya!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema katika kumbu kumbu ya miaka sitini tangu alipozaliwa, Baba Mtakatifu Francisko amempatia zawadi kubwa kwa kushirikisha furaha yake na ile furaha ya Familia ya Mungu nchini Ufilippini, walipokuwa wanakutana na Wakleri, Watawa na Majandokasisi.

Anasema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Ufilippini, ilikuwa ni kiboko chake, hajawahi kuona umati mkubwa wa watu wakishiriki kikamilifu katika mapokezi na maadhimisho mbali mbali ya Ibada zilizoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko. Hii inaonesha kwamba, kweli Familia ya Mungu nchini Ufilippini ina upendo mkubwa kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba na Rafiki wa maskini. Amewatia moyo watu waliotikiswa na janga la Yolanda na kwamba, wamejionea wenyewe mshikamano na upendo wa kidugu ulioneshwa na wananchi wa Ufilippini pamoja na kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa.

Kardinali Parolin anasema, katika hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Ufilippini, ameguswa kwa namna ya pekee na ushuhuda wa imani na matumaini uliotolewa na vijana na familia walipokutana na Baba Mtakatifu; mambo ambayo yamemtajirisha pia katika maisha na utume wake. Tufani ya Yolanda iliharibu miundo mbinu, lakini imani ikabaki thabiti.

Kardinali Parolin anasema, hali ilikuwa ni tofauti kabisa nchini Sri Lanka, ambako idadi ya Wakristo ni asilimia 6% ya idadi ya wananchi wote wa Sri Lanka, lakini ni waamini walionesha moyo wa Sala na Ibada; upendo na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Sri Lanka bado ina makovu ya vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu kwa takribani miaka thelathini, changamoto kwa sasa ni kuganga na kuponya madonda ya chuki na uhasama, tayari kujikita katika mchakato wa haki, amani, upatanisho, msamaha na umoja wa kitaifa, kama ambavyo ameelezea Rais mpya wa Sri Lanka wakati alipokutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko.

Kanisa linapenda kukazia umuhimu wa mchakato wa upatanisho unaojikita katika ukweli na uwazi; upendo na mshikamano; haki na msamaha wa kweli; ili wananchi waweze kuwa na ujasiri wa kuanza hija ya upatanisho na umoja wa kitaifa. Ndiyo maana anasema Kardinali Parolin Madhabahu ya Madhu ni kielelezo muhimu sana katika umoja, upatanisho na msamaha kati ya wananchi wa Sri Lanka. Hapa ni mahali pa sala, msamaha na upatanisho kati ya waamini wa dini mbali mbali nchini humo.

Kardinali Parolin anasema, Kanisa na watu wenye mapenzi mema wanalaani kwa nguvu zote vitendo vya kigaidi, vita na mashambulizi yanayofanywa kutokana na misimamo mikali ya kiimani. Ndiyo maana Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa dini mbali mbali kukemea na kulaani kwa macho makavu vitendo vya kigaidi kwani ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa. Kanisa bado linapenda kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini ili kujenga na kuimarisha ushirikiano, umoja na udugu miongoni mwa watu wa dini mbali mbali. Amani ya kweli inamwadabisha adui: kiroho na kimwili anasema Mtakatifu Ignasi wa Antiokia.

Kardinali Parolin anasema, kuna cheche za matumaini ya kuimarisha mahusiano kati ya Vatican na China, kwani kwa mara ya pili sasa Baba Mtakatifu anapita katika anga la Jamhuri ya Wananchi wa China. Kanisa linaendelea kusali na kujibidisha, ili siku moja, China na Vatican waweze kukutana katika ukweli na upendo, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu nchini China; katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, haki na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.