2015-01-20 08:02:56

Papa Francisko Barani Asia akazia: Heshima, maskini na familia!


Hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Asia kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 19 Januari 2015 imeendelea kuwa ni gumzo katika vyombo vya habari sehemu mbali mbali za dunia, lakini imekuwa ni changamoto ya kimissionari inayojikita katika maneno makuu matatu: heshima, maskini na familia. Hizi ni mada ambazo Baba Mtakatifu amezijadili kwa kina na mapana wakati wa hija yake ya kichungaji Barani Asia.

Vita, migogoro, chuki na kinzani ni mambo ambayo yanaweza kutatuliwa kwa kujikita katika mafao ya wengi sanjari na kuheshimu utu wa binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Watu wajenge utamaduni wa majadiliano katika uhuru, ukweli na uwazi, daima wakitafuta mafao ya wengi. Dini kamwe isiwe ni chanzo cha vita na kinzani ndani ya jamii, bali nguvu inayowaunganisha watu, changamoto ya kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo na udugu hata katika tofauti za kiimani.

Baba Mtakatifu katika hija yake Barani Asia amekazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa watu kujikita katika misingi ya haki, amani, utu na heshima ya binadamu. Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu. Kuna haja ya kusimama kidete kupinga mambo yote yanayopelekea ongezeko la umaskini wa hali na kipato; mambo ambayo kimsingi yanapata chimbuko lake katika ubinafsi, uchu wa mali na madaraka. Kuna haja kwa maskini kuthaminiwa na kuheshimiwa kama binadamu.

Baba Mtakatifu anasema, tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinakabiliwa na changamoto kubwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kuna nguvu ya giza inayoandama maisha ya ndoa na familia kwa kutaka kukumbatia utamaduni wa kifo, ili kutema Injili ya Uhai. Lakini binadamu anapaswa kukumbuka kwamba, ubinadamu unarithishwa kwa njia ya familia, kumbe familia haina budi kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.