2015-01-20 16:07:02

Mkutano wa Papa na waandishi wa Habari


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu jioni alirejea Roma baada ya safari ya muda wa saa 14 na dakika 40 angani, akitokea mji wa Manila hadi Roma, kwa ndege ya Shirika la Philippine Arilines. Hii ilikuwa ni ziara ya Saba ya Kitume kwa Papa Francisko, ambayo pia ilikuwa ni ziara ya pili kwake kutembelea bara la Asia, Safari ya kwanza alikwenda Korea. Na sasa kwa muda wa wiki nzima iliyopita 12 -19 Januari 2015, alikuwa Sri Lanka na Ufilipini.

Akiwa njiani kurejea Roma, alipata muda wa kubarizi na wanahabari na kujibu maswali yao kumi na mawili waliyo uliza. Maswali yaliyogusa maeneo mbalimbali tangu uwazi katika maisha, familia, na changamoto mbalimbali za kimaisha, Kikanisa na kijamii, kama rushwa, itikadi za ukoloni, nadharia za kijinsia na mpango wa uzazi . Aidha wanahabari walitaka kujua ziara anazotarajia kufanya mwaka huu 2015.

Papa akijibu swali, nini kimebakia akilini mwake, kama kumbukumbu kutoka Ufilipino , alitaja ni hisia na utendaji wa kweli usio na unafiki, wala kuwa kama maigizo, walioonyesha watu wa Ufilipino. Papa alisema , amelichukua hilo kama hazina itakayo mwongoza katika utendaji wake. Imani waliyoonyesha watu wa Ufilipino, imani iliyotoka kweli moyoni mwao watu hawa ambao licha ya kupitia mateso mbalimbali yakiwemo maafa bado waliweka tumaini kubwa kwa Mungu. Papa alikumbuka kwa jinsi walivyomlaki, jinsi walivyoonyesha imani yao, furaha yao ya kweli, baba wakiwainua watoto wao juu kwa juu, ili waweze kupokea baraka, na wale walio bubujikwa na machozi ya furaha kwa kukutana nae. Alisema, upendo ni wa hali ya juu ambao hajawahi kuushuhudia.

Papa alieleza kwa kutaja ishara mbalimbali zilizo onyesha upendo huu kutoka kwa akibaba, akinamama, shauku, furaha ya kweli ya watu , ambao pia wamepita mateso ya kweli , lakini mateso yao wameyaweka juu ya furaha ya kweli na matumiani mapya. Pia alimkumbuka kwa masikitiko binti aliyefariki kwa janga la hali mbaya ya hewa wakati wa maandalizi ya jukwaa Tacloban, akisema alifariki katika huduma ya Kanisa.
ziara kwa mwaka 2015
Papa alijibu swali jingine lililotaka kujua lini atakuwa na ziara barani Afrika, baada ya kuwa na ziara mbili barani Asia, wakati hajatembelea hata mara moja barani Afrika, ambako pia watu wanateseka kwa mengi, kama ilivyo Jamhuri ya Afrika Kati , Nigeria, Uganda. Ambako licha ya ghasia na mivutano ya kisiasa yenye kuzua machafuko ya mpigano na vita , pia waamini wengi wanateswa na umaskini wa kukithiri, uhafidhini wa Waislamu walisiovumilia wengine hasa ulioongezeka katika miaka ya hivi karibuni, pia majanga asilia na maradhi .
Alijibu, mpaka sasa kinadharia, anafikiria kwenda Jamhuri ya Afrika Kati na Uganda kwa mwaka huu,ikiwezekana kuelekea mwishoni mwa mwaka. Lakini itategemea pia majira ya nyakati, maana isingekuwa vyema kufanya ziara yake nyakati za mvua. Hivyo mipango iko jikoni ikipikika na inahitaji muda wa kuweka yote sawa.

Aidha Papa ametaja kumekuwa na ucheleweshaji wa ziara, pia kutokana na hali halisi za matatizo mengine kama ugonjwa wa ebola, ambao ni wazi huenea kwa kasi sana. Kwa kuwa ziara zake hukutanisha watu wengi mahali pamoja ni jambo la busara kujali pia usalama wa afya za watu. Pamoja na hali hizo, Papa Francisko alionyesha nia yake kwamba bila shaka mwaka huu, ataweza kutembelea Afrika. Na pia akataja nia yake ya kutembelea mataifa matatu ya Ametika ya Kusini kwa mwaka huu. Na kama mipango itakwenda kama inavyo andaliwa, ana hamu ya kutembelea Ecuador, Bolivia na Paraguay. Na kwa mwaka ujao anapenda kutembelea Chile, Argentina na Uruguay, lakini yote bado yanapikika jikoni.

Migogoro ya maskini
Na kwa nini ni vigumu hata kwa viongozi wa Kanisa kuukataa ubinafsi wa kujilimbikia mali na maisha mazuri wakati jirani zao wanaishi katika hali ngumu za umaskini wa kukitihiri, maisha yenye kuwa na pengo kubwa kati ya wenye navyo na wasiokuwa navyo, kama walivyoshuhudia pia wakati wakielekea uwanja wa ndege huko Sri Lanka? Pengine hali hiyo ndiyo inazua uwepo wa makundi ya kigaidi katika jamii? Papa alisema, kugawana na maskini chochote kinacho patikana, ndiyo wito na ujumbe mkuu wa kanisa leo hii.

Kanisa ni lazima kuwa na utambuzi kwamba, Maskini ni kafara wa utamaduni huu wa kupenda mambo ya dunia chimbuko la kubaguana.Papa alieleza na kuonya mwelekeo wa kutojali wengine , kama vile utu wao hauna thamani sawa, wanaochukuliwa kama ni taka za kutupwa nje, wanao nyanyasika kutokana na umaskini wao, wakilala nje ya majengo na thamani ya utu ikidharirika. Papa alieleza kwa masikitiko na kurejea alicho sisitiza akiwa Sri Lanka, ambako alikemea vikali rushwa na ubadhilifu kwamba, ni vyanzo vya maovu na huumiza vibaya umma wa kawaida.

Papa alirudia kukemea matendo maovu kama rushwa, ufisadi na ubadhilifu, kwamba uovu huu, ni "tatizo la kimataifa, ni ubinafsi wenye kuwaweka watu wengi katika hali ya umasikini wa kukithiri ambamo hawawezi kujinasua kiurahisi. Papa amelitaka kanisa kuwa mfano bora katika namna ya kukataa kuyapenda mambo ya dunia, yenye kugandamiza wengine na kuwacha katika hali mbovu. Ameasa hasa wote walioweka maisha yao wakfu, Maaskofu, Mapadre, Watawa, kutomezwa na hamu hizi za kutaka kujikusanyia mambo ya kidunia, lakini badala yake, wawe kioo cha kuonyesha jinsi ilivyo vyema kuwa mtu wa kawaida, katika hija ya maisha yenye kuandamana na Yesu.

Maisha ya kawaida kutembea wote kwa pamoja bila kuzidiana sana , huo ndiyo moyo wa Jumuiya hii inayoitwa Kanisa, vinginevyo haiwi tena Kanisa, lakini inakuwa ni taasisi ya kidunia, kama " NGO". Hilo si Kanisa la Yesu lakini ni NGO ya Kidunia kwa kuwa Kanisa ni kitu kingine tofauti. Kanisa la Kristo ni lile ambalo Kristo alikufa na kufufuka kwa ajili ya wokovu wetu, na wafuasi wa kweli bna aminifu kwa Kanisa wanapaswa kushuhudia hilo.

Papa alieleza juu ya mahangaiko ya watu maskini, na kutoa shukurani zake za dhati kwa mashirika na watu binafsi wanaokataa maisha ya kujilimbikizia wenyewe, watu wanaojiweka mbali na mambo ya kidunia badala yake wanajitolea kugawana walicho nacho na maskini, na katika hudumia .








All the contents on this site are copyrighted ©.