Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 25 Januari 2015
yatafanyika kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Mababa wa Kanisa cha Waagostiani, kilichoko
mjini Roma. Haya ni maadhimisho ya kiekumene yanayoratibiwa na Baraza la Kipapa la
Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume.
Kanisa linatambua kwamba, majadiliano
ya kiekumene ni sehemu ya mchakato wa maisha na utume wa Kanisa, mambo msingi yanayotekelezwa
na watawa katika maisha na huduma zao kwa Familia ya Mungu. Hiki ni kielelezo makini
cha Fumbo la Mwili wa Kristo yaani, Kanisa, safari makini ya kiekumene.
Maadhimisho
haya yanafanyika wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kuombea umoja wa Wakristo, kiasi
kwamba, watawa kutoka Makanisa ya: Kikatoliki, Kiorthodox, Kianglikani na Kiluteri
watashirikisha uzoefu na mang’amuzi yao katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene.
Maadhimisho haya yatakuwa yanafungwa kwa Sala ya Masifu ya Jioni, muda wa saa 1: 00
Usiku, kwa saa za Ulaya.
Jumapili tarehe 25 Januari 2015, majira ya saa 11:30
za jioni, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Masifu ya Pili ya Jioni kwenye
Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo nje ya kuta za Roma katika maadhimisho ya Siku kuu ya
kuongoka kwa Mtakatifu Paulo. Baba Mtakatifu katika barua yake kwa watawa kama sehemu
ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa anawahimiza watawa kukutana na kusali kwa pamoja
na watawa wa Makanisa mengine ya Kikristo, ili kukoleza moyo na ari ya mchakato wa
majadiliano ya kiekumene; kwa kufahamiana, kuheshimiana na kushirikiana kwa pamoja,
ili majadiliano ya kiekumene katika maisha ya kitawa yawe kweli ni msaada mkubwa katika
mchakato wa hija ya umoja wa Makanisa yote!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.