Serikali ya Tanzania inamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kulipandisha
Jimbo la Dodoma kuwa ni Jimbo kuu na hivyo kuupatia hadhi zaidi Mkoa wa Dodoma ambao
ni Makao makuu ya Tanzania. Dodoma ni kati ya Majimbo makuu matano yanayounda Kanisa
Katoliki la Tanzania. Jimbo hili lilitangazwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo
tarehe 6 Novemba 2014 na kumteua Askofu Beatus Kinyaiya kuwa Askofu mkuu wa Jimbo
kuu la Dodoma.
Kuundwa kwa Jimbo kuu la Dodoma ni kielelezo makini cha kukua
na kuimarika kwa imani na baraka kwa Familia ya Mungu Jimboni humo, changamoto ya
kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa,
kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wote!
Hii ni sehemu ya hotuba
iliyotolewa na Dr. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania mara baada ya Ibada ya kumsimika Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu
la Dodoma, Jumapili, tarehe 18 Januari 2015, kwenye Viwanja vya Kanisa kuu la Mtakatifu
Paulo wa Msalaba, Jimbo kuu la Dodoma.
Serikali ya Tanzania inalishukuru na
kulipongeza Kanisa Katoliki kwa mchango wake uliotukuka katika sekta ya elimu, afya
na ustawi wa jamii na kwamba, limekuwa mstari wa mbele katika kuisaidia Serikali kupambana
na umaskini, ujinga na maradhi maadui wakuu wa Tanzania. Kanisa limewekeza sana katika
utunzaji bora wa mazingira, kama sehemu ya mchakato wa kuboresha maisha ya watanzania
wote.
Makamu wa Rais ambaye alikuwa anashangiliwa na umati mkubwa inatokana
na ufundi aliouonesha wa kunukuu vifungu vya Biblia, katika hoja zake na kwamba, Kanisa
Katoliki nchini Tanzania ni sawa na tawi la mzabibu ambalo limeshikamana na Yesu Kristo
anayeliwezesha kuzaa matunda mengi katika medani mbali mbali za maisha ya Watanzania.
Mchango unaotolewa na madhehebu na dini mbali mbali nchini Tanzania ni mkubwa na kwamba,
Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote katika mchakato wa maboresho ya maisha
ya watanzania wengi!
Askofu mkuu Beatus Kinyaiya katika nembo yake kama Askofu
mkuu anakazia amani na mshikamano; mambo ambayo Makamu wa Rais anasema ni msingi thabiti
katika maendeleo na ustawi wa binadamu wote; changamoto kwa watanzania kuhakikisha
kwamba, wanadumisha: haki, amani, upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa na kukataa
katu katu kutumbukizwa katika kishawishi cha udini, ukabila na umajimbo, mambo ambayo
hayana tija wala mashiko kwa maendeleo na ustawi wa Watanzania: kiroho na kimwili.
Makamu
wa Rais anasema, amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kulindwa
na kutetewa na wananchi wote na wala si dhamana ya wanasiasa peke yao! Waamini wanahamasishwa
kuwa ni wachamungu, kutafuta kwa bidii kuwa na amani na watu wote, huku wakichuchumilia
utakatifu wa maisha, ili shina la uchungu lisije likachipua na kuwasumbua katika maisha
yao. Watanzania waendelee kuombea amani pamoja na kuitetea, kwa kutambua kwamba, wao
wote ni watoto wa Mwenyezi Mungu.
Makamu wa Rais amewakumbusha waamini wa dini
mbali mbali nchini Tanzania kwamba, ni dhambi kubwa kukashfu dini au imani ya jiani
zao. Na mtu yeyote anayefanya hivyo atambue kwamba, anavunja Katiba ya Nchi ambayo
kimsingi ni sheria mama na atashughulikiwa na vyombo vya dola. Amani inajengeka na
kustawi mahali penye upendo, huruma na msamaha; mahali ambapo ubinafsi, chuki na uhasama
hauna nafasi katika mioyo ya watu; wananchi wajitahidi kuushinda ubaya kwa kutenda
mema.
Makamu wa Rais anasema kwamba, chaguzi mbali mbali zitakazofanyika nchini
Tanzania kwa Mwaka 2015 ni mwaliko kwa wananchi kufanya maamuzi sahihi, ili kuwachagua
watu safi watakaoiongoza nchi; kwa kuangalia sifa kuu za kiongozi kuwa ni mtu anayetambua
kwamba, uongozi ni huduma na wala si kwa vile mtu anajisikia kutaka kuingia madarakani
kupitia kwa migongo ya wanyonge. Serikali imejipanga barabara kuhakikisha kwamba,
amani na utulivu vinalindwa na kudumishwa, ili kuwapata viongozi watakaoshirikiana
na wananchi kujiletea maendeleo yao wenyewe.