2015-01-19 08:50:02

Walei!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo. Kwa mara nyingine tena tunakukaribisha uendelee kukitegea sikio kipindi chetu pendevu, ili tuisikie sauti ya Mama Kanisa anayetuelekeza nini cha kufanya ili Kanisa lizidi kuwa hai na Injili ya Kristo isonge mbele kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. 00:09:55:27 RealAudioMP3

Baada ya kuongelea Maaskofu, Mapadre na Watawa katika vipindi vilivyopita, leo tunawatupia jicho waamini walei kwa kuutazama utume wao ndani ya Kanisa na kwa ulimwengu, kama tusomavyo katika hati ile iitwayo kwa lugha ya Kilatini ‘Apostolicam Actuositatem’ yenye kumaanisha Utendaji wa Kitume.

Tutakumbuka kwamba, Mtaguso Mkuu wa II wa Vatican ndiyo uliotoa sura mpya ya Kanisa, yenye kulionesha kanisa kama Watu wa Mungu, Familia ya Mungu au Mwili wa fumbo wa Kristo. Hayo yote yalikuwa ni kujaribu kuonesha Kanisa kama Muungano kamili wa Wabatizwa wote, ambapo tunaishi na tunasafiri pamoja katika hija yetu ya hapa duniani. na lengo la u-pamoja wetu ni kusaidiana, kuimarishana, kutegemezana, kutakatifuzana, kuyatakatifuza malimwengu na sisi wenyewe kuendelea kufanywa watakatifu. Wajibu huu ni wa waamini wote na una msingi katika Ubatizo wetu.

Ndiyo maana katika Hati hii, Mtaguso wa pili wa Vaticani uliwaongelea walei kwa namna ya pekee na ukionyesha nafasi yao katika maisha ya . Hati hii ni mwongozo wa Utume wa Walei katika Kanisa na Ulimwengu. Mtaguso unasema, sisi waamini walei, tuna nafasi kubwa sana ya kushiriki katika utume wa Kanisa katika nyanja mbalimbali, kama vile katika familia zetu, katika Jumuiya za Kanisa, katika mazingira mbalimbali ya kijamii na pia katika maeneo yetu ya kazi, ambako twaweza kupeleka cheche za Injili ya Kristo kwa maneno na matendo na zaidi sana kwa mfano wa ushuhuda wa maisha yetu ya kila siku, yenye kutoa mirindimo ya Injili ya Kristo.

Katika nyanja hizo, sisi walei tunatumwa kutekeleza utume wa kuinjilisha na wa kutakatifuza, kukoleza zaidi roho ya Kikristo katika ulimwengu na kuzidisha zaidii matendo ya huruma. Ni kwa njia hiyo nasi walei tutakuwa tunamfuasa Kristo anayesali, anayefundisha, anayewahurumia na kuwasaidia wenye shida na anayeeshiriki maisha yake na ulimwengu.

Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ulitazama kwa kina na kuona kwamba, asilimia kubwa ya waamini wote wa ni walei, tena ndio wanaoshirikiana zaidi na watu wowote katika mambo mengi. Hivyo wasipotoa mchango wao, utume wa Kanisa utadumaa. Mwamimi mlei kwa hulka yake na uwezo wake na kwa fursa ya mazingira ya maisha yake, ana nafasi kubwa sana ya kuuinjilisha Ulimwengu. Akitekeleza wajibu huo kwa moyo na kwa kushirikiana na miongozo mbalimbali ya Kanisa, hapo kazi ya Uinjilishaji itasonga mbele.

Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican unatuelekeza, ili kweli sisi walei tuweze kutimiza utume wetu vizuri, tujibidishe kwanza kabisa kuurutubisa Ukristo wetu uliojengeka katika ubatizo kwa kukoleza maisha yetu ya kiroho, maisha yetu ya muungano binafsi na Mungu. Huu ni mwito wa kila siku kujaribu kuuambata uongofu wa kweli. Ni kwa njia hiyo, tutaweza kutekeleza utume wa kuwasaidia wengine pia.

Mtaguso unasisitiza kwamba, utume wetu sisi walei, sio tu kueneza ujumbe wa , bali pia kuratibu malimwengu yafuate , kutimiza matendo ya na kushuhudia . Nyakati zetu hizi zinashuhudia hali ya aibu katika kushuhudia Injili ya Kristo, na wakati mwingine watu kushindwa kuwianisha tunu za Injili wanazozisadiki na maisha halisi ya utendaji ya kila siku. Kiujumla ni kushindwa kuyamwilisha mafundisho ya Kristo katika maisha yetu ya kila siku.

Na kibaya zaidi, kunazidi kukua roho ya ubinafsi-angamivu, ambapo tunashuhudia vitendo vya biashara haramu ya binadamu, utumwa mamboleo, biashara za bidhaa za vitu hatarishi na angamizi kwa usitawi wa binadamu, upandikizwaji wa vita na magonjwa kati ya watu, upandikizwaji wa itikadi na mifumo angamizi kwa mustakabali wa familia ya mwanadamu; haya na mengineyo mengi kama hayo, ni dalili za kukosekana kwa utume makini wenye kuzaa matunda kati ya watu.

Tunasema hivyo kwa sababu wanayotenda hayo, baadhi yao ni sisi tunaomsadiki Kristo. Kwa mwangwi wa hati hii, mwito kwetu sote kupenyeza roho ya Kikristo katika maisha yetu ya kila siku na katika mazingira yote ya watu.

Mtaguso unatueleza pia namna za kutimiza utume huo, kuanzia ule kwa mtu mmojammoja hadi ule wa pamoja katika vyama mbalimbali ambavyo walei wana haki ya kujiundia, na katika miundo maalumu iliyoanzishwa na wachungaji wao au wanayojianzishia wenyewe kwa kufuata taratibu za Kanisa. Kila mtu kwa nafasi yake anaalikwa kufanya utume kwa kutangaza injili na kutakatifuza, iwe ni kwa mtu mmoja au kwa kundi la watu. Na pia inahimizwa sana kutekeleza utume huo katika umoja, kwa njia ya vyama vya kitume. Vyama vya kitume ni msaada mkubwa sana katika kujiendeleza sisi wenyewe kiroho na pia katika kuunganisha nguvu zetu za uinjilishaji wa kina kwa pamoja.

Mtaguso unatuelekeza pia utume huo tuutende kwa utaratibu wenye kuongozwa na roho wa Mungu, na sio katika roho ya na mashindano bali kwa upendo na , kwanza na maaskofu, mapadre na wahudumu wengine mpaka na wa tofauti na wasio Wakristo.

Mpendwa msikilizaji, mara nyingi wivu na mashindano yenye majivuno, vimekuwa ni baadhi ya mambo yanayokwamisha kabisa kazi ya Injili. Mahali penye wivu, kazi ya Mungu hukwama kwa sababu, watu tunatumia muda mwingi kuoneana wivu, kusemanasemana, kuharibiana kazi, kutafutatafuta makosa, badala ya kufanya mambo ya msingi. Mashindano yenye harufu ya ubinafsi, kujitutumua, kutafuta umaarufu na sifa, na kudharau wengine, kunyanyapaa wanyonge na maskini, navyo vimekuwa ni kikwazo kikubwa sana katika utume wa walei. Lengo la utume wetu sisi walei ni kushiriki katika kazi ya ukombozi wa mwanadamu kimwili na kiroho.

Sisi walei tutekeleze utume wetu ndani ya Kanisa kwa namna ya kufikiri pamoja na Kanisa na kutenda kadiri ya Miongozo ya Kanisa. Tukiwa tayari kutoa ushirikiano mnyoofu kwa viongozi wetu wa Kiroho, na sisi wenyewe tukijibidisha kutekeleza yale tunayopaswa kutenda, hapo utume wetu utakuwa hai zaidi na zaidi. Daima tufungue macho, ili kwa mwanga wa Injili tuone ni maeneo yapi haswa tunapaswa kupenyeza Injili ya Kristo zaidi na zaidi.

Hati hii inahitimishwa kwa kusisitiza sana malezi bora ya utotoni na ujanani. Roho ya utume ndani ya Kanisa hufundishwa na kupandikizwa tangu utotoni. Hivyo watoto wasiachwe nyuma na Vijana nao waangaliwe kwa umakini. Malezi ya kiutu na Kikristo yapatiwe mkazo zaidi. Hayo husaidia sana kumuunda mtu anayefaa na anayejali utu. Malezi ya kitaaluma peke yake, pasipo utu wala dhamiri hai kwa Mungu, ni hatari kwa watoto wetu.

Ninakualika mpendwa mwamini mlei, kufufua na kukuza sana ile roho ya uwajibikaji ndani ya Kanisa na katika mazingira yote yalioainishwa. Mahali popote tuwapo, tuwe wakristo hai, na kwa roho ya umoja na uwajibikaji wa kweli, tutimize wajibu wetu vema.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.