2015-01-18 08:13:15

Watu wengi hawana ujasiri wa kulia tena!


Baba Mtakatifu Francisko, ameianza Siku ya Jumapili tarehe 18 Januaria 2015 kwa kuzungumza na umati mkubwa wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za Ufilippini, kwenye Chuo kikuu cha Mtakatifu Thoma, kwa kumkumbuka kijana Chrystel aliyekuwa anafanya kazi ya kujitolea kwenye Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, nakufariki dunia wakati wa maandalizi ya jukwaa kwa ajili ya Ibada ya Misa Takatifu mjini Tacloban, Ufilippini. Baba Mtakatifu amepata nafasi pia ya kuzungumza na Baba mzazi wa Marehemu Chrystel kwenye Ubalozi wa Vatican mjini Manila.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa vijana amekazia mambo makuu matatu: umuhimu wa vijana kujikita katika maadili na utu wema; kulinda na kutunza mazingira pamoja na kuwahudumia maskini. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuhakikisha kwamba, daima wanatafuta kilicho kweli, chema na kizuri kwa kuachana na tabia ya ubinafsi, chuki na ukosefu wa uaminifu, kwa kuwa mashuhuda waaminifu kwa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake pamoja na kujenga mahusiano mazuri na jirani.

Vijana wasikubali kutumiwa au kutumia vijana wengine kwa ajili ya faida binafsi, bali wajifunze kupenda na kudumisha maadili na utu wema, hata kama watachekwa na wengine. Vijana wajenge utamaduni wa kusali na kushiriki mara kwa mara Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili kweli waweze kuwa ni mfano bora wa kuigwa na vijana wenzao, chemchemi ya matumaini kwa wale wanaokumbwa na kishawishi cha kuacha masomo na kuingia mtaani ili kuganga njaa kwa siku moja!

Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza vijana waliotoa ushuhuda wao katika nyanja mbali mbali za maisha na kusema kwamba, bado mfumo dume unaendelea kutawala kwani wasichana wamewakilishwa kwa idadi ndogo ikilinganishwa na wavulana. Swali la msingi lililoulizwa, inakuaje leo hii kuna umati mkubwa wa watoto wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia? Baba Mtakatifu anasema, kuna watu ambao hawana tena huruma na mapendo kwa watoto. Ni Kristo peke yake anayeweza kulia kwa kufahamu kile kinachoendelea katika maisha ya binadamu!

Leo hii watu wengi wanakosa ujasiri wa kulia kwa huruma kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Watu wanaokula, wakashiba na kusaza hawana sababu ya kulia, changamoto ya kujiuliza kama hata wao katika maisha yao wameguswa na huruma kiasi cha kudondosha machozi wanapomwona mtoto anayeteseka kwa njaa na utapiamlo; kijana aliyeathirika kwa kutumia dawa haramu za kulevya; watoto wasiokuwa na makazi; wanaoishi katika mazingira hatarishi; wanaodhalilishwa na kunyanyaswa?

Kuna watu wanaojifanya kana kwamba, wanahuruma na huzuni, lakini wanataka kuwatumia watoto na vijana hawa kwa ajili ya mafao yao binafsi, haya ndiyo "machozi ya mamba". Baba Mtakatifu anawataka vijana kujifunza kuwa na huruma! Yesu alionesha huruma kwa kumlilia rafiki yake Lazaro, akamhurumia yule mwanamke aliyekuwa amempoteza mwanaye wa pekee kwa kumfufua na kumpatia tena; akawahurumia watu waliokuwa wanatangatanga pasipokuwa na mchungaji. Huruma ndiyo changamoto kubwa inayopaswa kushuhudiwa na Wakristo duniani.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumzia kuhusu njia za mawasiliano anasema, zina faidi kubwa kwa kuwawezesha vijana kuwa na ufahamu mkubwa wa mambo mengi, lakini hawawezi kuutumia vyema kwa ajili ya mafao yao, Kanisa linawahitaji vijana wema na watakatifu na wala si majumba ya makumbusho! Vijana wenye uwezo wa kupenda kwa kujifunza maana halisi ya maisha na hivyo kumwilisha ujuzi na maarifa katika uhalisia wa maisha yao. Haya ni mambo yanayojikita katika kufikiri, kusikia na kutenda.

Baba Mtakatifu anasema, binadamu ana uwezo wa kupenda na kupendwa na kwamba, ni rahisi sana mtu kupendwa, kuliko kupenda na kwamba, upendo mkamilifu ni Mungu mwenyewe, anayewataka waja wake kumwachia nafasi ili aweze kuwaonesha pendo lake kuu na kuendelea kuwashangaza, ili waweze kujikita katika majadiliano ya kweli kwa yule anayependa na kupendwa. Mfano wa Mathayo mtoza ushuru, aliyeonja upendo wa Yesu, akaacha yote na kumfuasa Kristo, watu waliokuwa wanamfahamu wakapigwa na bumbuwazi!

Baba Mtakatifu anasema, Mathayo alitoa kipaumbele cha pekee kwa Yesu na kumwonesha kwamba, alikuwa na thamani kubwa machoni pake kuliko hata utajiri aliokuwa nao kibindoni; huu ndio mshangao anaoufanya Mwenyezi Mungu kwa binadamu. NI mshangao ambao Mwenyezi Mungu aliweza kumkirimia Mtakatifu Francisko, kijana tajiri, aliyefariki dunia pasi na mali, lakini moyo wake ukiwa umesheheni utajiri mkubwa! Vijana waendelee kujifunza mengi, lakini pia wawe na busara ya kumwachia Mungu nafasi ya kuendelea kuwashangaza katika maisha!

Baba Mtakatifu anawataka vijana kujifunza kusaidia na kusaidiwa na Yesu, ili kutambua mambo msingi katika maisha kama alivyomwambia yule kijana tajiri kwamba, unapungukia jambo moja! Nenda kauze vyote ulivyo navyo, kisha njoo unifuate!

Baba Mtakatifu anawataka vijana kujifunza kutoka kwa maskini na wale omba omba wa mitaani, wanaopokea kwa unyenyekevu mkubwa kile wanachopatiwa, changamoto na mwaliko kwa vijana kuwa ni Wainjilishaji miongoni mwa maskini na kuendelea kuwajifunza katika maisha yao, kwani wanayo mambo mengi yanayoweza kuwatajirisha.

Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, wao pia ni maskini wanaopaswa kuinjilishwa na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na wagonjwa, ili kuwawezesha kukua na kukomaa katika moyo wa huduma na sadaka kwa wengine. Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini linaadhimisha Mwaka wa Maskini, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujisadaka kwa ajili ya kuwapenda na kuwahudumia maskini katika uhalisia wa maisha na wala si katika ndoto au sera zinazobaki kwenye karatasi.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kulinda na kutunza mazingira kwa kutekeleza dhamana na wajibu huu kwa jicho la imani kwani mazingira ni sehemu ya kazi ya uumbaji na kuna uhusiano mkubwa na utu wa binadamu, kwani hawa wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kupewa dhamana ya kuitiisha dunia. BInadamu anawajibika kutengeneza dunia ili iweze kuwa ni bustani nzuri kwa ajili familia ya binadamu pasi na kuharibu misitu, ardhi au kuchafua vyanzo vya maji. Kila mwamini anawajibika kimaadili kulinda na kutunza mazingira, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Wachunguzi wa mambo wanasema, mkutano kati ya Baba Mtakatifu na Vijana nchini Ufilippini, umekuwa ni "kiboko yao", kwani ameweka pembeni makaratasi ya hotuba, akaanza kuwapangia vijana "matofali" yanayojikita katika maadili na utu wema; utunzaji wa mazingira na huduma kwa maskini. Vijana wamemzawadia Baba Mtakatifu Francisko kasha la salam na matashi mema kutoka kwa vijana wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Thoma wa Akwino, Manila.

Askofu Leopoldo Jaucian, Mwenyekiti wa Tume ya Vijana, Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini, amemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, vijana wanamwona kuwa ni Mchungaji mwema, anaonesha upendo na huruma kwa Kondoo wake, lakini zaidi kwa wale waliopotea. Kundi la vijana mbele yake linaonesha unyofu, mawazo, ndoto, karama na matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi, kwani wao ni zawadi kwa Kanisa na hazina ya ulimwengu.

Hili ni kundi la vijana wenye shida na mahangaiko mbali mbali katika maisha; wanataka kusikilizwa, katika shida na mahangaiko yao pamoja na kuimarishwa katika ndoto zao na kwamba, wana imani kubwa na Fumbo la Msalaba wa Kristo linaloonesha upendo na huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.