2015-01-18 10:12:27

Lindeni watoto na familia!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili mchana tarehe 18 Januari 2015 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Rizal Park, Jimbo kuu la Manila; ibada ambayo imehudhuriwa na bahari ya watu kutoka sehemu mbali mbali za Ufilippini. Kwa Ibada ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Papa amehitimisha hija yake ya kitume nchini Sri Lanka na Ufilippini aliyoianza tarehe 12 Januari 2015. Ni Ibada ambayo imejikita katika dhamana na utume wa Kanisa katika Umissionari na kwamba, Familia ya Mungu nchini Ufilippini, inatumwa kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake ameonesha kwa kina na mapana mahusiano yaliyopo kati ya Ufalme wa Mungu na utoto katika maisha ya kiroho, Habari Njema ya Wokovu; ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti sanjari na umuhimu wa mwanadamu kujikita katika mchakato wa kutunza na kudumisha: haki, amani na wajibu. Kila Mkristo anachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba anajenga na kudumisha Ufalme wa Mungu kama kielelezo cha utambulisho wao wa Kikristo; kielelezo makini kilichooneshwa na Familia ya Mungu nchini Ufilippini, ndugu zao walipofikwa na majanga ya tufani ya Yolanda.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Ufilippini ni nchi ya kwanza ya Kikristo Barani Asia; zawadi kubwa ya Mungu na baraka kwa watu wake, inayowawajibisha kama sehemu ya wito wao wa Kikristo, ili kuwa kweli ni mashuhuda na wamissionari mahiri wa imani Barani Asia.

Kwa njia ya dhambi ya asili, binadamu ameharibu uzuri na kuvunjilia mbali umoja na mshikamano wa Familia ya binadamu, kwa kujenga na kuanzisha miundo mbinu ambayo ni chanzo kikuu cha umaskini, ujinga, rushwa na ufisadi. Maandiko Matakatifu yanabainisha kwamba, tishio kubwa la Mpango wa Mungu kwa mwanadamu daima umekuwa ni uwongo. Shetani ni baba wa uwongo anayejificha kwa mambo yenye mvuto na mashiko katika mwonekano wake wa nje kama mambo mapya yanayowatambulisha na wengine katika jamii.

Baba Mtakatifu anasema, Shetani anawavuta watu kwa mambo yanagusa vionjo vyao vya ndani, raha na starehe za mpito, kiasi kwamba, watu wanaharibu zawadi na karama mbali mbali ambazo wamejaliwa na Mwenyezi Mungu; kwa kuchezea maisha na kupoteza fedha kwa kucheza kamari sanjari na ulevi wa kupindukia, kiasi cha mwanadamu kuharibu maisha yake. Mtu anashindwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mambo msingi katika maisha, katika hali ya unyenyekevu na hekima kama watoto wadogo, kinyume kabisa na walimwengu! Huu ni ujumbe unaopaswa kumgusa kila mwamini katika undani wake wa maisha kwa kutambua kwamba, waamini wanaitwa kuwa ni Familia ya Mungu.

Mtakatifu Nino anawakumbusha waamini kwamba, utambulisho huu hauna budi kulindwa na kuendelezwa. Mtoto Yesu ambaye ni Mlinzi wa nchi ya Ufilippini anaendelea kuwahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema, umuhimu wa kulinda na kutunza familia, Kanisa na Familia ya Mungu ambayo kimsingi ni familia ya binadamu wote.

Baba Mtakatifu anasema, leo hii kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kutetea familia kwani inakabiliwa na mashambulizi pamoja na programu ambazo kimsingi ni kinyume kabisa cha Mafundisho ya Kanisa ambayo yanajikita katika wema na utakatifu. Waamini wanao wajibu na dhamana ya kulinda, kuongoza na kuwatia ari na moyo vijana pamoja na kuwasaidia kujenga jamii inayojikita katika amani ya maisha ya kiroho na kitamaduni.

Kanisa linapenda kuona kwamba, kila mtoto ambaye ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu anapokelewa, anapendwa na kutunzwa. Kuna haja ya kuwahudumia vijana, ili kamwe wajanja wachache wasiwapokonye matumaini yaliyomo ndani mwao kwa kuwatelekeza katika mazingira hatarishi na hatimaye, kuishia barabarani.

Ni mtoto dhaifu aliyetekeleza mapenzi ya Mungu, kwa kuonesha huruma na haki duniani. Akaonesha uaminifu mkubwa na kukataa kishawishi cha rushwa; urithi wa dhambi; akashinda dhambi na mauti kwa nguvu ya Fumbo la Msalaba.

Mara baada ya Ibada ya Misa takatifu, Askofu mkuu Socrates B. Villegas, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini, amemshukuru Baba Mtakatifu kwa mwanga angavu aliowaletea na kwamba, mwanga huu, kamwe hautafifia katika maisha yao. Tangu alipowasili nchini Ufilippini, amewaonjesha watu furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na kwamba, wataendelea kuwa ni mwanga wa upendo na huruma ya Kristo kwa waja wake, ili kuwasha moto wa Injili ya Furaha ulimwenguni. Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini linamshukuru Baba Mtakatifu kwa kuwa kweli Mwenyezi Mungu anawapenda na kuwajali!

Naye Kardinali Luis Antonio Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila, amemshukuru Baba Mtakatifu kwa kuwajali na kuwakumbatia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kuendelea kusimama kidete kutetea haki na amani duniani pamoja na utunzaji bora wa mazingira. Familia ya Mungu nchini Ufilippini inamwahidia Baba Mtakatifu sala, ili kamwe asitindikiwe na imani, matumaini na mapendo kama Yesu alivyomwambia Mtakatifu Petro.

Waamini na watu wenye mapenzi mema, wanataka kumsindikiza Baba Mtakatifu anapokwenda pembezoni mwa jamii, ili kuwasalimia na kuwahudumia wale wanaoishi katika umaskini na mazingira magumu; wagonjwa. Wanataka kumsindikiza anapowainjilisha wanasiasa, wachumi, wanasayansi, wanautamaduni na vyombo vya upashanaji habari, ili wote hawa waweze kuona mwanga wa Kristo ambaye amekuwa ni kiini cha hija yake ya kitume nchini Ufilippini. Uwanja huu maarufu kwa Serikali na Kanisa; ni mahali ambapo Wamissionari wapya wanatumwa kueneza mwanga wa Yesu, daima wakiwa wameungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.