2015-01-17 10:20:14

Kumbe, si wapweke kamwe!


Rais Benigno Simeon wa Ufilippini katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini Ufilippini, ili aweze kuzungumza na viongozi wa Serikali na Wanadiplomasia, Ikulu mjini Manila, Siku ya Ijumaa, tarehe 16 Januari 2015, amemshukuru na kumpongeza kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko, kuwa ni sauti ya kinabii, inayowaunganisha na kupyaisha maisha watu wote wenye mapenzi mema!

Rais Simeon anasema, Baba Mtakatifu Francisko amekuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kusimama kidete kulinda na kuwatetea maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; ushuhuda unaojikita katika uhalisia wa maisha yake. Rais amekumbushia shida na magumu aliyokumbana nayo katika safari yake kama mwanasiasa, kiasi cha familia yake kutengwa na wengi wakati wa utawala wa mabavu nchini Ufilippini.

Katika kinzani na magumu nchini Ufilippini, wengi walinyamazishwa, ni viongozi wa Kanisa walioonesha ujasiri wa kukemea nyanyaso na madhulumu dhidi ya wananchi wa Ufilippini; Wakleri wakaonesha kuwa kweli ni kielelezo cha wachungaji wema; wakasimama kidete kulinda na kuimarisha imani ya Familia ya Mungu nchini Ufilippini; wakajenga umoja na mshikamano wa kidugu, leo hii ni familia moja inayowajibika na kutaabikiana katika raha na magumu ya maisha.

Rais Simeon anasema, wanasiasa hawana budi kujikita katika mchakato wa kutafuta na kusimamia mafao ya wengi ndani ya jamii, kila mtu akijitahidi kuwajibika na kamwe wasiwe ni watu wanaopandikiza mbegu ya chuki na kinzani kati ya wananchi. Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa wasaidizi wake wakuu alikuwa amekazia umuhimu wa kuondokana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kujenga na kuimarisha moyo wa furaha katika huduma, ili kujenga na kudumisha Ufalme wa Mungu hapa duniani.

Ni maneno ambayo Rais Simeon anasema yanaonesha ujasiri wa Baba Mtakatifu katika ukweli na uwazi, changamoto hata kwa wanasiasa kujivika ujasiri huu katika huduma kwa wanannchi wanaowahudumia. Serikali ya Ufilippini katika mapambano ya kuleta mageuzi nchini humo, inatambua kwamba, kuna kundi kubwa la watu ambalo linawaunga mkono, kumbe, si wapweke kamwe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.