2015-01-17 14:14:08

Juma la kuombea umoja wa Wakristo!


Jumapili ya wiki hii, 18 Januari hadi Jumamosi ijayo 25 Januari 2015, ni juma zima la kuombea umoja wa Wakristo. Ni juma la kushiriki katika juhudi za pamoja kwa ajili ya kuombea Umoja wa Kanisa, kama wajibu kwa Kanisa zima, wote waamini na wachungaji wake. RealAudioMP3

Na kila aliyebatizwa kwa jina la Kristo , anaalikwa kuungana na Wakristo wenzake, kutolea sala na maombi, kushirikishana na kukaribishana mmoja kwa mwingine, kadri ya uwezo wake, iwe kupitia njia ya maisha ya kawaida ya kila siku, pia kutoa ushuhuda wenye kuonyesha wazi umoja wa Wakristu kimatendo si kwa maneno tu. Ni kushiriki katika ibada za pamoja kiteolojia na matendo mema, kama alivyosema Yesu alipokutana na Mwanamke Msamaria, kisimani, “ Nipe Maji ninywe”..

Katika wiki hii, tunaalikwa sote tulenge kuonyesha uhusiano wetu katika kiungo kimoja kinacho tuunganisha kama wafuasi wa Kristo aliye mmoja tu, hoja inayo sukuma madhehebu mbalimbali ya Kikrsito, kujenga umoja kamili na timilifu kulingana na fadhili za Mungu. Wiki hili ni juhudi zinazotoa mwaliko wa kuondokana na ukritiba wa kale wa kubaguana , umimi Mkatoliki , mimi mluteri, mimi Mpentecoste , mimi mlokole, mimi mimi mimi, bali iwe kujumuika pamoja kama wana wa Bwana Mmoja Yesu Kristo.

Mwaka huu, Wiki ya Kuombea Umoja wa Wakristo, inaongozwa na Kauli mbiu, Yesu akamwambia, "Nipatie maji ninywe." Taz.Yohana 4: 7. Mada hii ilichaguliwa na kuandaliwa ujumbe wa Wawakilishi kutoka Baraza la Kitaifa la Makanisa ya Kikristo ya Brazil (CONIC). CONIC, ilichagua mada, na kuipeleka katika Kamati ya Kimataifa, iliyofanya mkutano wake São Paulo, Brazil, wajumbe wake wakiwa kutoka Tume ya Makanisa ya Baraza la Makanisa la Dunia WCC na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Kukuza Umoja wa Wakristo.

Waandaaji wa Wiki hii ya sala ya Kuombea Umoja wa Wakristo, wanafafanua kwa nini walichagua mada hiyo wakisema, Yesu kukutana na Mwanamke Kisimani na kusema nipe maji ninywe, ni tukio linalotoa mwaliko kwa Wakristo wote , kujaribu kuteka maji kutoka kisima tofauti na kile walicho kizoea, kisima ambacho hawakielewi sana . Hii ina maana ya kushiriki ibada za wengine, ni kutazama utendeji wa madhehebu mengine, na kuchota yote yaliyo mema kama hatua ya kuimarisha zaidi Ukristo wetu. Na kwamba katika utofauti wetu, mna utajiri mwingi wa karama za kiroho, tunaoweza jifunza kwa manufaa ya maisha yetu ya Kikrsto. Humo tunaweza kuimarishana mmoja kwa mwingine.

Yesu alipomwambia mwanamke, "tafadhali nipe maji ninywe, hili ni tamko la kimaadili, linaloonyesha utambuzi kwamba , binadamu hajitoshelezi peke yake lakini hutegemeana moja kwa mwingine, hata katika kuuishi utume wa kanisa. Ina maana ya sisi kubadili mtazamo wetu, na kuwajibikaji zaidi katika kuutafuta umoja kamili kati ya tofauti nyingi, kupitia uwazi wetu katika aina na mifumo mbalimbali ya maombi na sala kwa Kikristo.

Hivyo wiki la kuombea Umoja wa Kikristo,inakuwa ni Upendeleo wa kipekee wenye kutuzamisha katika maombi ya pamoja, kukutana na mazungumza na wengine. Ni fursa ya kujielimisha zaidi juu ya utajiri na thamani ya uwepo wa aina nyingine za karama katika kumtukuza Mungu , kuabudu, kutolea maombi kwake.

Ni wiki ya kumwomba Mungu, zawadi hii ya umoja kwa wafuasi wote wa mwanae, kama Yesu mwenyewe alivyotamani na kuomba; , Bwana naomba hawa ulio nipatia, ili wawe wamoja kama sisi tulivyo na umoja.

Wiki la kuombea umoja wa Wakristo si tukio lililoanza miaka ya hivi karibuni lakini miaka imetembea tangu liliponzishwa, kumwomba Bwana , zawadi hii ya umoja wa wafuasi wa mwanae. Nyaraka zinaonyesha tarehe 18-25 Januari ilipendekezwa mwaka 1908, na Paul Wattson, Mwanzilishi wa Chama cha Upatanisho wa binadamu na Mungu , kama kuunganisha maadhimisho ya Sikukuu ya Kiti cha Mtume Petro (Januari 18) na kuongoka kwa Mtume Paul (Januari 25) katika umuhimu wao. Na hivyo tangu wakati huo Mama Kanisa hutembea katika barabara hiyo.

Waandaaji wanaendelea kusema, tunaishi katika ulimwengu wenye alama nyingi za utofauti katika lugha, utamaduni, na hata mazingira na hali ya hewa, na hivyo tunapaswa kueleza imani yetu ya Kikristo kwa njia tofauti. Kuuishi utofauti huu, kwa wito aminifu kwa Kristo, tunapaswa kuwa kitu kimoja , umoja wa kanisa lake, kama ulivyo mwili wa mtu, ni mmoja lakini una viungo mbalimbali.

Kanisa Katoliki katika hati yake juu ya Uekumene (Unitatis Redintegratio), limeandika, Wiki la Sala kuombea Umoja wa Wakristo , lengo lake ni kuhamasisha urudishaji wa Umoja kati ya Wakristo. Kristo Bwana alianzisha Kanisa moja na pekee , ingawa udhaifu wa bindamu umeligawa kanisa katika madhehebu dhehebu licha kwamba, wote hujieleza mbele ya watu, kuwa ni urithi halisi wa Yesu Kristo, na wote wanakubaliana kwamba ni wafuasi wa Bwana mmoja , ingawa na wana fikra tofauti katika njia zao za kumfuata Kristo, tofauti tofauti, kana kwamba Kristo amegawanyika . Na hivi Mtaguso wa Pili wa Vatican , umeonya , hiki ni kikwazo kwa ulimwengu na hudhuru tendo takatifu la kuhubiri Injili kwa kila kiumbe.

Hata hivyo, pamoja na udhaifu huu wa kibindamu, bado Kanisa katika hali yake ya kuwa limegawanyika vipandevipande , linaisikia sala ya Yesu kwa kanisa lake, inayonyesha hamu kwa wafuasi wake, kuwa na umoja. Sala hiyo inaendelea kulisindikiza Kanisa kwa hekima na saburi. Na hivyo popote duniani Wakristo wanasukumwa na hamu na neema hii ya kuutafuta umoja kamili kati ya ndugu walio tengana , wakijihusisha katika harakati za kurudisha umoja huo, kupitia njia mbalimbali , kama ilivyo katika Wiki hii ya kuombea Umoja wa Wakristo.

katika wiki hili, tukiwa Wakristo, bila kujali madhehebu yetu tunahimizwa kukumbuka kwamba, kwa kadri tunavyojibidisha kuyatafuta maisha matakatifu , kufuatana na Injili, ni kadri hiyohiyo , tunahamasisha na kutekeleza umoja wa Wakristo. Kwa kuwa kwa kadri tunavyokuwa katika usharika na Mungu Baba, Neno na Roho , ndivyo tutakavyo weza kukuza udugu kati yetu kwa udani zaidi na kwa urahisi zaidi, kama Wakaristo.

Na hivyo ushirikiano na umoja katika sala, wenye kuchochewa na uongofu wa moyo na utakatifu, kama mmoja mmoja na kama jumuiya kwa ajili ya kuombea umoja wa Wakristo , vinapaswa kupewa kipaumbele katika harakati zote za kiekumeni . Juhudi hizi zinahimizwa kuwepo mara kwa mara kama Bwana wetu Yesu Kristo alivyotamani na kuomba kwa Baba kabla ya kifo chake , Baba naomba ili wote wawe na Umoja .

Ombi la Kristo linatutaka Wakristo wote kama mwli mmoja kukiri mbele ya Mataifa imani yetu kwa Mungu mmoja mwenye nafsi tatu. Umoja huu na iwe ishara wazo kwa mataifa, yenye kuuonyesha mwili mmoja wa Kristo, wenye kuwa na viungo mbalimbali vyenye kutegemeana. Na hiyo ndiyo tafsiri ya Kauli mbiu ya wiki hii la kuombea Umoja wa Wakristo kwa mwaka huu, "nipe maji ninywe". Ni mada inayoonyesha kugawana na wengine neema na karama alizojaliwa kila mmoja. Kwa ushirikiano huu wa kukutana na wengine, na tuombe kupata yale tunayopungukiwa bila kuogopa, na wenye kuwa navyo wagawie wengine bila ubaguzi , kama ilivyokuwa katika tukio la Yesu kukutana na mwanamke Msamaria kisimani.
Kumbe basi, tunapoitikia wito huu wa kwenda kushiriki katika Ibada zilizoandaliwa kwa ajili ya kuombea umoja wa Wakristo tunatimiza hamu ya Yesu mwenyewe aliyeomba , “Baba naomba, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo na umoja” . Mungu atubariki sana.
imeandaliwa na TJ Mhella.








All the contents on this site are copyrighted ©.