Askofu msaidizi Daniel Adwok wa Jimbo kuu la Khartoum Sudan, ambaye hivi karibuni
alitembelea katika maeneo ambayo bado yanawaka moto wa vita ya wenyewe kwa wenyewe
Sudan ya Kusini, amekazia umuhimu wa majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya pamoja
na kujenga moyo wa upendo na mshikamano kwa wakimbizi na wahamiaji, ambao wanatafuta
hifadhi ya maisha yao badala ya kuwatelekeza.
Askofu msaidizi Adwork, akiwa
katika maeneo haya, ameweza kukaa na kuzungumza na viongozi wa Serikali, viongozi
wa Kanisa, wakimbizi na wahamiaji, ambao walimpokea kwa moyo wa shukrani kwa kuwasikiliza
na kuwajali katika mahangaiko yao. Amewakumbusha wananchi wa Wilaya ya Maban ambao
miaka kadhaa iliyopita walilazimika kuyakimbia makazi yao ili kutafuta hifadhi Kaskazini
mwa Sudan au Nchini Ethiopia. Kumbe, kuna haja ya kujenga na kuimarisha utamaduni
wa ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji. Wilaya ya Maban kwa sasa inatoa hifadhi kwa
wakimbizi na wahamiaji wapatao 130, 000 kutoka Blue Nile.
Askofu msaidizi Adwok
pia ametembelea na kukagua miradi mbali mbali inayoendeshwa na Shirika la Wayesuit
kwa ajili ya kuwahudumia Wakimbizi, JRS kwa kukazia umuhimu kwa Mashirika ya misaada
ya Kanisa Katoliki kuhakikisha kwamba, yanaangalia kwa makini mahitaji ya wakimbizi
na wananchi mahalia, ili kujenga na kudumisha amani kati ya makundi haya mawili.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.