Jopo la Madaktari wasiokuwa na mipaka linasema kwamba, bado kuna watu wengi Kaskazini
mwa Nigeria walioshambuliwa na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram, wanakabiliwa na
upungufu mkubwa wa chakula unaotishia ongezeko la utapiamlo miongoni mwa watoto, kuna
watu ambao wameathirika sana kutokana na mashambulizi haya na kwamba, bado watu hawana
uhakika wa usalama wa maisha yao, kumbe wanahitaji huduma ya tiba na chakula!
Wananchi
waliopata majeraha makubwa kutokana na mashambuli yaliyofanywa huko Baga hivi karibuni
wanaendelea kupata matibabu huko Maiduguri na kwenye eneo la Ziwa Chad. Inasemekana
kwamba, kuna bado watu ambao wamejificha msituni kwa kuhofia usalama wa maisha yao.
Jopo la Madtkari wasiokuwa na mipaka hivi karibuni baada ya kuangalia mahitaji
msingi, limetoa msaada wa chakula, dawa na vifaa tiba, ili kuokoa maisha ya wahanga
wa shambulizi la Baga, ambalo viongozi wengi wa kidini wanasema, kuna haja kwa Jumuiya
ya Kimataifa kuonesha mshikamano wao wa dhati ili kupinga vitendo vya kigaidi, vinavyoendelea
kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.
Katika kipindi cha miaka mitano
Boko Haram imekuwa ni tishio kubwa kwa usalama wa wananchi na mali zao. Kimeendelea
kuwatumia watoto wadogo kwa ajili ya mabomu ya kujitoa mhanga, kutekwa makundi makubwa
ya watu pamoja na kufanya mashambulizi. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya wakimbizi
laki nane hadi millioni moja wanaoishi Kaskazini Mashariki wa Nigeria.