2015-01-16 08:34:26

Sikilizeni kilio cha maskini!


Baba Mtakatifu Francisko ameanza rasmi hija yake ya kitume nchini Ufilippini, siku ya Ijumaa asubuhi kwa kupokelewa kwa heshima, akapigiwa mizinga ishirini na moja, akazungumza na Rais wa Ufilippini Bwana Benigno Simeon pamoja na familia yake pamoja na kuweka sahihi kwenye kitabu cha wageni mashuhuri ambako amemtakia Rais na watu wake neema, hekima, ufahamu, ustawi na maendeleo. Baadaye akapata pia fursa ya kuzungumza na viongozi wa kisiasa pamoja na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao Ufilippini.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia kwamba, hii ni hija ya kichungaji na kitume ambayo ni sehemu ya mchakato wa maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 500 tangu Ukristo ulipoingia na kuota mizizi nchini Ufilippini, tukio ambalo litafikia kilele chake kunako mwaka 2021. Huu ni muda mrefu ambao Ukristo umechangia kwa kiasi kikubwa katika utamaduni wa wananchi wa Ufilippini. Lakini Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, hija hii pia ni kutaka kuonesha mshikamano wake wa dhati kwa wananchi walioguswa na kutikiswa na tufani ya Yolanda, iliyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Baba Mtakatifu anapongeza moyo wa mshikamano uliooneshwa na wananchi wa Ufilippini, lakini zaidi miongoni mwa vijana katika kukabiliana na maafa asilia. Hii ni fadhila ambayo imejikita katika imani ya Kikristo, iliyomwilishwa katika wema na ukarimu na ndiyo maana Baba Mtakatifu anapenda kuonesha mshikamano na ukaribu na watu wote wa Ufilippini waliofikwa na maafa asilia.

Fundisho la mshikamano ni muhimu sana kwa ajili ya siku za usoni: kama familia kila jamii inachota nguvu humo ili kukabiliana na changamoto za maisha. Ufilippini kama zilivyo nchi mbali mbali Barani Asia, inakabiliwa na changamoto za mabadiliko katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya jamii ya kisasa, inayoheshimu na kuthamini tunu msingi za kiutu, inayolinda utu na haki ya kila binadamu, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Yote haya ni mambo muhimu sana katika kukabiliana na misimamo mipya ya kisiasa na na kimaadili.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wanasiasa kutekeleza dhamana yao kwa kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi; kwa kuhifadhi rasilimali watu na vitu; mambo ambayo kwa hakika Mwenyezi Mungu ameikirimia nchi ya Ufilippini. Hii ni changamoto ya kujenga mazingira muhimu ili vijana wa kizazi kipya waweze kujenga jamii inayojikita katika misingi ya haki, mshikamano na amani. Utekelezaji wa malengo ya kitaifa unakwenda sanjari na misingi ya kimaadili inayomwilishwa katika haki jamii pamoja na kuheshimu utu wa binadamu.

Baba Mtakatifu anasema, kadiri ya Mapokeo ya Maandiko Matakatifu, yanakazia umuhimu wa jamii kusikiliza kwa makini kilio cha maskini wanaokabiliwa na kashfa mbali mbali zinazojionesha katika ukosefu wa usawa kijamii. Mageuzi katika miundo mbinu ya kijamii inayochangia kuenea na kutengwa kwa maskini, inahitaji kwanza kabisa wongofu wa moyo na akili, ndiyo maana Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini linaadhimisha Mwaka wa Maskini.

Hii ni sauti ya kinabii inayowaalika watu wote kutafakari na hatimaye kufanya marekebisho katika hatua mbali mbali za maisha ya kijamii; kwa kusimama kidete kupinga rushwa na ufisadi pamoja na mambo yote yanayochangia umaskini na tabia ya kuwatenga maskini katika jamii.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, kiini cha hija yake ya kitume nchini Ufulippini ni kukutana na kuzungumza na familia pamoja na vijana. Familia ina dhamana na utume maalum katika jamii: ni katika familia kwamba, vijana wanajifunza tunu msingi za maisha ya kiutu na kimaadili katika mazingira halisi kwa maisha yao yote. Familia haina budi kuimarishwa na wala si kuharibiwa wala "kuichakachua". Hii inatokana na ukweli kwamba, demokrasia mamboleo inakabiliwa na magumu mengi katika kuheshimu utu wa kila binadamu; haki msingi ya watoto ambao bado hajawazaliwa, wazee na wagonjwa.

Katika mazingira kama haya anasema Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa viongozi wa kisiasa na wanadiplomasia nchini Ufilippini, familia na jamii husika hazina budi kutekeleza dhamana yake msingi kwa kujenga utamaduni unaowashirikisha watu katika wema, mshikamano na uaminifu mambo msingi katika maadili yanayoiwezesha jamii kuishi kwa pamoja.

Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa kuonesha mchango wa Ufilippini katika masuala ya ushirikiano wa kimataifa Barani Asia, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa watu wenye shida wanaoishi ughaibuni au diaspora kwa kuchangia ustawi wao. Baba Mtakatifu anaendelea kuwahamasisha viongozi wa Ufilippini kuhakikisha kwamba, kila mwananchi anapata uhakika wa maendeleo yake: kiroho na kimwili, sanjari na kuendeleza mchakato wa majadiliano na ushirikiano kati ya waamini wa dini mbali mbali.

Baba Mtakatifu anaonesha matumaini yake kwa hatua mbali mbali zilizokwisha kufikiwa katika kuimarisha na kuendeleza amani Kusini mwa Ufilippini; mambo ambayo yatasaidia kutoa suluhu ya haki mintarafu kanuni msingi za nchi ya Ufilippini; kwa kuheshimu watu wote bila ubaguzi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP. S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.