2015-01-16 08:36:35

Shikamaneni na maskini ili kuwajengea imani na matumaini mapya!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 16 Januari 2015 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Wakleri, Watawa na Majandokasisi kutoka nchini Ufilippini pamoja na wawakilishi kutoka katika nchi mbali mbali Barani Asia, kwani hija hii ni kwa ajili ya Bara la Asia katika ujumla wake. Ibada hii imefanyika kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Jimbo kuu la Manila.

Katika mahubiri yake kwa namna ya pekee kabisa Baba Mtakatifu ameitaka Familia ya Mungu nchini Ufilippini kuonesha upendo wa dhati kwa Kristo pamoja na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, kwani hawa ni hazina kubwa ya Injili. Amewakumbusha viongozi wa Kanisa pamoja na watawa kwamba, ufuasi na upendo wao kwa Kristo unasaidia kukuza mchakato wa upatanisho.

Kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 500 ya Ukristo nchini Ufilippini, yatakayofikia hatima yake kunako mwaka 2021, Baba Mtakatifu anasema kwamba, kizazi kilichopita kimesaidia kwa kiasi kikubwa watu kufahamu Neno la Mungu, tunu msingi za maisha ya Kikristo, ambazo zimemwilishwa katika huduma ya mapendo, upatanisho, mshikamano na mafao ya wengi. Tunu hizi zimeimarisha si tu wakati wa mahubiri au ujenzi wa Kanisa nchini Ufilippini, bali pia zimesaidia kumwilisha Injili ya Upendo, msamaha, mshikamano na huduma kwa ajili ya mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anawaalika vijana wa kizazi kipya kuhakikisha kwamba, wanajenga madaraja yatakayolisaidia Bara la Ulaya kupokea Neno la Mungu. Watu hawana budi kuonesha upendo kwa Kristo anayewaletea upatanisho wa kweli. Mchakato wa kukutana na Yesu hauna budi kuwakirimia waamini wongofu pamoja na kuchunguza dhamiri kama mtu binafsi na jamii katika ujumla wake. Injili ya Kristo haina budi kusaidia mchakato wa ujenzi wa jamii imara inayojikita katika msingi wa haki na kukombolewa.

Baba Mtakatifu anawapongeza Maaskofu Katoliki nchini Ufilippini wanaosimama kidete kupambana kufa na kupona na mambo yanayosababisha ukosefu wa haki na usawa katika jamii. Injili inamchangamotisha kila mwamini kuhakikisha kwamba, anaishi kwa kuzingatia misingi ya uaminifu, ukweli pamoja na kujisadaka kwa ajili ya mafao ya wengi. Injili inawataka Wakristo kujenga na kudumisha makundi ya watu waaminifu; wenye kushikamana pamoja na kujitoa kwa ajili ya kuleta mageuzi ndani ya jamii kwa njia ya ushuhuda wa kinabii.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kuiangalia changamoto hii, anawataka kwa namna ya pekee, Wakleri na watawa kujenga utamaduni wa kusali kila siku kama sehemu ya mchakato wa kukutana na Kristo pamoja na kupambana kufa na kupona, ili kukataa kishawishi cha kutaka kumezwa na malimwengu; ubinafsi pamoja na kupenda mali badala yake, wawe ni watu wanaojisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jirani zao; watu wakweli na waaminifu; wanaosaidia ustawi na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili; tayari kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kueneza Injili katika jamii inayojikita kwenye ubaguzi, mvuto usiokuwa na mashiko pamoja na kashfa ya ukosefu wa misingi ya usawa.

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kutoa kipaumbele cha pekee kwa Mapadre vijana, watawa na majandokasisi, ambao walikuwa wamefurika kwa wingi katika Ibada hii ya Misa Takatifu, wanaoweza kuchanganyikiwa n akukata tamaa, lakini bado wanaendelea kuliona Kanisa kama mwenzi katika hija ya maisha yao na chemchemi ya furaha. Kanisa linapaswa kuwa karibu zaidi na wale wote wanaoelemewa na umaskini, rushwa na ufisadi, kiasi cha kujikatia tamaa, kiasi hata cha kuingiwa na kishawishi cha kuacha masomo na kujitosa barabarani.

Baba Mtakatifu anawataka Wakleri kutangaza uzuri na ukweli wa ndoa ya Kikristo katika jamii ambamo kuna mambo mengi ambayo yanaendelea kuwachanganya watu kuhusiana na maisha ya ndoa na familia. Huu ni ukweli ambao unakabiliwa na changamoto nyingi, zinazotaka kuathiri mpango wa kazi ya uumbaji na kupotosha ukweli wa tunu msingi za maisha zilizounda na kujenga uzuri wa utamaduni wa Ufilippini.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake kwa Wakleri, Watawa na Majandokasisi kwa kusema kwamba, miaka 500 ya Ukristo nchini humo si haba, kwani imesaidia kujenga upendo mkubwa kwa Mwenyezi Mungu, Ibada kwa Bikira Maria na Rozari Takatifu, muhtasari wa Injili. Hapa kuna nguvu kubwa inayoweza kusaidia mchakato wa umissionari unaopaswa kusaidia utamaduni wa Kikristo miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, ili ari na moyo wa Kikristo uweze kupenya na hatimatimaye kuota mizizi katika jamii ya Wafilippini na kwa njia yao, jamii nyingine sehemu mbali mbali za dunia.

Naye Kardinali Luis Antonio Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, ametambua uwepo wa uwakilishi wa Familia ya Mungu kutoka Barani Asia. Kanisa kuu la Manila ni kielelezo makini cha wananchi wa Ufilippini, Kanisa ambalo limekumbana na majanga mbali mbali katika historia, lakini bado liko imara; Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa. Furaha ya wananchi wa Ufilippini inajikita katika muziki na imani inayowawezesha kusimama tena na kusonga mbele baada kukumbwa na majanga mbali mbali katika maisha.

Kardinali Luis Antonio anasema, uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko kati yao ili kuwaletea moto unaowatakasa; tetemeko linalowaamsha, anawaletea silaha ili kuwalinda na kuendelea kulijenga Kanisa la Kristo sanjari na kuwaimrisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo.

Mara tu baada ya Ibada ya Misa Takatifu, Papa Francisko amekwenda kuwatembelea na kuwaslimia watoto wanaoishi katika mazingira magumu wanaotunzwa na Kituo cha TNK kilichoanzishwa na Padre Mathieu. Baba Mtakatifu amezungumza na watoto hawa, akapiga nao picha za kumbu kumbu na baadaye wakampatia zawadi ya Sanamu ya Bikira Maria na zawadi nyingine, mwishoni, anasema Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican, Baba Mtakatifu akawabariki na hatimaye kuendelea na ratiba yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.











All the contents on this site are copyrighted ©.