Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi afariki dunia kwa ajali
Askofu Joseph Mukasa Zuza wa Jimbo Katoliki Mzuzu, nchini Malawi ambaye pia alikuwa
ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi, Alhamisi, tarehe 15 Januari 2015 amepata
ajali ya gari na kufariki dunia.
Rais Peter Mutharika wa Malawi ametuma salam
za rambi rambi kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi kwa kukumbwa na msiba huu mzito.
Rais Mutharika anaungana na waamini pamoja na wananchi wote wa Malawi wanaoomboleza
msiba wa Askofu Joseph Mukasa Zuza; kiongozi aliyeonesha moyo wa uzalendo na kusimamia
mafao ya wengi wakati Malawi ilipokuwa inapitia kipindi kigumu katika historia yake.
Ni kiongozi aliyejisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wake, akawa
ni mshirika na mdau mkuu wa ushirikiano na Serikali katika kuwahudumia wananchi wa
Malawi. Ni kiongozi aliyekuwa sauti ya kinabii kwa kuwatetea wanyonge na wale wote
waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Atakumbukwa kutokana na huduma yake kwa
Familia ya Mungu, Malawi.