Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, Alhamisi tarehe 15 Januari 2015 inawaalika waamini na
watu wote wenye mapenzi mema kushikamana kwa njia ya sala kwa ajili ya kuwakumbuka
na kuwaombea watu ambao wanaendelea kupoteza maisha yao nchini Nigeria kutokana na
mashambulizi ya kigaidi, ambayo kwa sasa yameingia katika mtindo wa hatari kwa kutumia
watoto wadogo wanaojitoa mhanga ili kuwaangamiza ndugu zao.
Ibada hii ya sala
inatarajiwa kuongozwa na Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la
familia, kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria in Trastevere, mjini Roma. Takwimu zinaonesha
kwamba, zaidi ya watu elfu mbili wameuwawa kikatili kutokana na mashambulizi ya kikundi
cha kigaidi cha Boko Haram na kwamba, kuna umati mkubwa wa watu ambao umelazimika
kuyakimbia makazi yake kwa kuhofia usalama wa maisha.
Jumuiya ya Mtakatifu
Egidio, Jumapili iliyopita imeshiriki pia katika maandamano ya amani mjini Paris,
Ufaransa, kupinga vitendo vya kigaidi vinavyotishia umoja na utofauti wa wananchi
wa Ulaya pamoja na juhudi za kuimarisha uhuru wa kujieleza. Lakini, Jumuiya ya Mtakatifu
Egidio yenye makao makuu mjini Roma na ambayo imekuwa mstari wa mbele katika mchakato
wa upatanisho sehemu mbali mbali za dunia, imeikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kwamba,
kuna watu wasiokuwa na hatia nchini Nigeria wanaendelea kupoteza maisha yao kutokana
na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na Boko Haram, kumbe hata Nigeria inapaswa kuungwa
mkono na Jumuiya ya Kimataifa kama ilivyofanya kwa Ufaransa iliposhambuliwa na magaidi
hivi karibuni.
Mkutano huu wa sala unaongozwa na kauli mbiu "Sisi sote ni
Wanaigeria". Mashambulizi ya kigaidi nchini Nigeria hayabagui wala kuchagua, kumbe,
kuna haja ya kuonesha mshikamano wa dhati kwani kuna umati mkubwa wa waamini wa dini
ya Kiislam ambao unajikita katika majadiliano, maridhiano na amani katika ya watu.
Kundi hili linapaswa kuungwa mkono, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi
pa kuishi kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu na kwamba, tofauti za kidini
zisiwe ni chanzo cha karaha na maafa kati ya watu.
Waamini na watu wenye mapenzi
mema wanasali kwa ajili ya kuombea mchakato wa ushirikishwaji wa wahamiaji na wageni
uendelee kwa kuzingatia misingi ya utu na heshima ya binadamu. Kusiwepo tena mtu au
kundi la watu linalojihusisha na mashambulizi ya kigaidi kwa kisingizio cha kidini.
Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inapenda kuikumbusha Jumuiya ya Kimataifa hatari kubwa
iliyoko nchini Nigeria na nchi ambazo ziko katika Ukanda wa Sahara zinavyotishiwa
usalama, ustawi na maendeleo yake kutokana na vitendo vya kigaidi.