2015-01-15 11:55:45

Karibu Ufilippini; uwaimarishe ndugu zako!


Baba Mtakatifu Francisko amewasili mjini Manila, Ufilippini siku ya Alhamisi tarehe 15 Januari 2015 na kupokelewa kwa heshima na taadhima na kwenye Uwanja wa Ndege wa Villamour, Manila. Umati mkubwa wa watu ulikuwa umejipanga kwenye viunga vya mji wa Manila, ili kumpokea na kumsalimia Baba Mtakatifu Francisko anapoanza hija yake ya kitume nchini Ufilippini.

Hii ni mara ya tano kwa Ufilippini kutembelewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Itakumbukwa kwamba, mara ya kwanza Ufilippini ilitembelewa na Mwenyeheri Paulo VI, miaka 45 iliyopita, baadaye Mtakatifu Yohane Paulo II akatembelea Manila kunako mwaka 1981 na mwaka 1995. Baba Mtakatifu anafanya hija hii kama kielelezo cha mshikamano na upendo kwa wananchi wa Ufilippini ambao wametikiswa vibaya sana na majanga asilia, kiasi cha kuendelea kuwatumbukiza watu wengi katika umaskini wa hali na kipato.

Kardinali Luis Antonio Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini mwao anataka kukutana na kuzungumza na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake; ni hija inayokazia majadiliano ya kidini na kiekumene kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya Barani Asia.

Kardinali Tagle anasema katika maandalizi ujio wa Baba Mtakatifu nchini humo, wamejitahidi kuwa na kiasi kwa kutambua mtindo na mfumo wa maisha ya Baba Mtakatifu Francisko, mtu asiyependa makuu! Anakuja kuwafariji ndugu zake katika shida na magumu, ili aweze kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo. Mapokeo ya Baba Mtakatifu ni changamoto inayowataka waamini na watu wenye mapenzi kujenga utamaduni wa kuwajali na kuwahudumia maskini na wahitaji.

Fedha itakayobakia katika maandalizi ya ujio wa Baba Mtakatifu itatumika kwa ajili ya kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anataka kuwaimarisha ndugu zake katika imani, kwa kuwasikiliza na kusali pamoja nao, kwa kutambua kwamba, umri wa Baba Mtakatifu pia umekwenda, kumbe anahitaji mapumziko. Kardinali Luis Antonio Tagle anasema, Baba Mtakatifu yuko nchini Ufilippini ili kukutana na Familia ya Mungu sanjari na kuwasikiliza maskini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.