2015-01-15 11:28:43

Dumisheni amani, utulivu na maendeleo!


Balozi wa Algeria ambaye amemaliza muda wake wa utumishi nchini Tanzania, Mheshimiwa Tabat Jallouh amewatakia Watanzania mwaka 2015 uwe ni mwaka wa mafanikio, amani na utulivu, kwa kadri nchi inavyopitia katika mabadiliko makubwa ya kisiasa kwa njia ya kura ya maoni ya Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu.
Mheshimiwa Jallouh alitoa salamu zake hizo kwa Watanzania usiku wa kuamkia, Jumatano, Januari 14, 2015, wakati alipokuwa anaagana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam.

Balozi Jallouh alimwambia Rais Kikwete kuwa anasikitika kuondoka mapema bila kuwa shuhuda na shahidi wa matukio hayo muhimu katika historia na uhai wa taifa la Tanzania.

“Nakutakia wewe binafsi, Mheshimiwa Rais na kupitia kwako, Watanzania wote, mwaka wenye utulivu, mafanikio na amani kwa kadri nchi inavyopita kipindi cha kutunga Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu. Ni matukio muhimu sana katika historia na uhai wa taifa la Tanzania,” alisema Balozi Jallouh, ambaye pia alimtakia Rais Kikwete maisha marefu na shughuli zenye mafanikio baada ya kustaafu.
Balozi Jallouh ambaye Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza Kusini mwa Jangwa la Sahara kuitumikia katika utumishi wake wa kibalozi, amekuwa Balozi wa Algeria katika Tanzania kwa miaka mitano.

Naye Rais Kikwete amemshukuru Balozi Jallouh kwa kuinua kwa kiwango kikubwa uhusiano wa Tanzania na Algeria. “Tunakushukuru kwa utumishi wako, tunakushukuru kwa kutuunga mkono, tumekuwa marafiki wa miaka mingi lakini wewe umetoa mchango wa pekee. Tutakukumbuka daima.”








All the contents on this site are copyrighted ©.