2015-01-15 11:29:29

Asanteni sana wananchi wa Sri Lanka!


Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kufunga vilago nchini Sri Lanka tayari kuanza safari kuelekea Manila, nchini Ufilippini, alitembelea na kusali kidogo kwenye Kikanisa kilichowekwa chini ya usimamizi wa Bikira Maria wa Sri Lanka katika kitongoji cha Bolawalana, Jimbo kuu la Colombo.

Hiki ni Kikanisa ambacho kiko katika Taasisi ya Kitamaduni ya Benedikto XVI, iliyoanzishwa kunako mwaka 2011 na Jimbo kuu la Colombo, ili kuimarisha mchakato wa ushirikiano kati ya Kanisa, Serikali na wadau mbali mbali, katika ujenzi wa Sri Lanka mpya baada ya miaka mingi ya vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Baba Mtakatifu ameagwa na viongozi wakuu wa Sri Lanka, akakagua gwaride la heshima na baadaye kuanza kuondoka kuelekea Manila, Ufilippini. Akiwa njiani, Baba Mtakatifu Francisko amewatumia salam na matashi mema viongozi wakuu wa Sri Lanka, India, Myanmar, Thailand, Cambodia na Vietnam.

Baba Mtakatifu amemshukuru kwa namna ya pekee Rais wa Sri Lanka kwa mapokezi makubwa na ukarimu ambao ameushuhudia kutoka kwa wananchi wa Sri Lanka na kwamba, anawahakikishia sala na sadaka yake kwa ajili ya amani,umoja ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Sri Lanka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.