2015-01-15 11:05:42

Amani ya kweli inajikita katika utu wa binadamu!


Maaskofu wanaoratibu misaada kwa Nchi Takatifu waliohitimisha hija yao ya mshikamano wa udugu na upendo huko Mashariki ya Kati,Alhamisi tarehe 15 Januari 2015, katika tamko lao wanasema kwamba, utu na heshima ya binadamu ni kiini cha amani ya kudumu, kinachoshinda kinzani na migawanyiko kati ya watu.

Maaskofu wanasema Uutu wa binadamu unapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, vita na kinzani zinazoendelea huko Mashariki ya Kati zina madhara makubwa kwa maisha ya wananchi wengi na kwamba, majanga yanayoendelea kwenye Ukanda wa Ghaza yanasababishwa na binadamu wenyewe. Hii ni kashfa inayoendelea kusababisha mateso na mahangaiko ya watu, kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro huu na kwamba, uwepo wa Maaskofu huko Mashariki ya Kati ni ushuhuda kwamba, Jumuiya ya Wakristo bado haijasahaulika.

Maaskofu wanasema, kuna maelfu ya wahamiaji na wakimbizi ambao wanateseka kwa kukosa makazi na watu wengi wamekata tamaa huko Ghaza. Wamejionea wenyewe Jeshi la watu wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji; wametembelea shule na kuona jinsi ambavyo watoto wanaishi kwa pamoja bila ya kujali imani zao. Maaskofu wameshuhudia na kuguswa na huduma inayotolewa na watawa katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu.

Wanasiasa wanalo jukumu la kulinda utu na heshima ya binadamu, mambo mengine wananchi watayapata kwa ziada na kwamba, ujenzi wa kuta zinazowatenganisha watu, una madhara makubwa, kwani utakwamisha uhuru wa watu. Maaskofu wanawasihi wadau kujikita tena katika majadiliano ya kisiasa yanayopania kupata ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro kati ya Israeli na Palestina na kwamba, kila upande unapaswa kutambua kwamba, Nchi Takatifu ni maskani ya dini kuu tatu na makazi kwa mataifa mawili.

Maaskofu katika tamko lao wanasema kwamba, amani ya kweli inajikita katika haki msingi za binadamu na kwamba, wao wataendelea kusali na kuwasaidia wananchi wa pande hizi mbili, ili amani ya kweli iweze kupatikana na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu katika Ukanda huu unaoitwa Nchi Takatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.