2015-01-14 11:26:40

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kawaida cha Mwaka!


Ninayofuraha kubwa hivi leo tunapojiunga pamoja nawe kutafakari Neno la Mungu chakula cha roho zetu. Dominika iliyopita tulisherehekea sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, sikukuu ambayo ilitualika kurudia ahadi za ubatizo wetu, na hivi kujiweka tayari kusonga mbele katika imani katika mwaka mpya. RealAudioMP3

Kama ilivyo kawaida sikukuu hiyo hufunga kipindi cha Noel na kuanzisha kipindi cha kawaida cha mwaka. Leo basi mpendwa tupo pamoja katika Dominika ya II ya mwaka.

Mpendwa msikilizaji, Neno la Mungu katika Dominika hii latusaidia kugundua namna Mungu anavyoita na namna gani tuitike. Kwa hakika Mungu humwita mtu kwa jina lake, ingawa huitwa kwa mafaa ya jumuiya na Kanisa kwa upana wake kiulimwengu.

Hivi Mungu amfahamu kila mmoja wetu kina, hakuna anayeweza kumdanganya Mungu. Mpendwa, Mungu aitapo huita kwa uvumilivu, hachoki na hivi hutaka mpaka mtu asikie sauti yake, ndiyo kusema hushika agano lake na msimamo thabiti katika ahadi zake. Mambo haya tunayajua kwa njia ya wito wa Samueli. Anamwita kwa jina na polepole Samueli anasikia sauti ya Bwana.

Ewe unayenisikiliza katika tafakari hii, sauti ya Mungu iitapo yadai kuitika na hivi Samueli ni mfano bora wa namna ya kuitika akisema “nena Bwana kwa kuwa mtumishi wako anasikia” Hii ndiyo sentensi ambayo wapaswa kuitamka kila siku ya maisha yako, tena ilingane na moyo wa ndani.

Ni wajibu wa ubatizo ambao tuliupokea mwanzoni mwa imani yetu na hata tukarudia ahadi za ubatizo katika sikukuu ya Ubatizo wa Bwana na kila siku katika Kanuni ya imani. Mpendwa tunahitaji maongozi ya kimungu ili tuweze kusikia vema sauti ya Mungu, na hivi kazi ya Eli aliyekuwa kuhani ilikuwa kumsaidia Samueli apambanue sauti ya Mungu toka sauti nyingine.

Leo hii Kanisa zima latusaidia kupambanua sauti ya Bwana. Mtakatifu Yohane Paulo II katika barua yake ya kichungaji iitwayo “Familiaris Consortio” juu ya Wajibu wa Familia za Kikristo anawaalika mapadre na wote wenye kushughulikia familia wakizingatia Maongozi ya Magisterium yaani mamlaka ya Kanisa wapambanue yote yaliyo mema toka mabaya katika kuzielekeza familia kwenye utakatifu. Katika hili, Kanisa lamwalika mmojammoja kuwa na mlezi wa kiroho anayesaidia kuongoza maisha ya Kikristo.

Mtume Paulo atuonya kama alivyowaonya Wakorinto kuwa mwili si kwa zinaa bali ni hekalu la Roho wa Bwana. Mwili ni zawadi kwa mwanadamu kwa ajili ya uumbaji na hivi yatupasa daima kukumbuka kuwa tunaitwa kutunza na kuheshimu mwili tuliokabidhiwa na Mungu. Kumbuka fumbo la umwilisho, Bwana alitaka kuutakatifuza mwili na hivi katika mlengo huo nasi twafanya hivyo.

Katika somo la Injili tunaalikwa katika wito tulioupokea kuwa kama Yohane Mbatizaji. Anamtambulisha Bwana na kisha anamwacha Bwana asonge mbele na kazi yake. Utume wa Yohane ulikuwa wa kutayarisha njia ya Bwana na sasa Bwana lazima akue na Yohane Mbatizaji apungue.

Je sisi twawaalika watu kwenda kwa Kristu au kwa ajili yetu wenyewe ktk ubinafsi wetu?, tafakari! Je twajiona wa maana zaidi kuliko wengine? Tunaalikwa basi hivi leo kutekeleza wito wetu kwa njia ya fadhila ya unyenyekevu.

Mitume wanapoongea na Bwana na wanagundua kuwa Bwana ni Masiha na wanasema tumemwona Masiha. Wanaitika na wanamwona Bwana kuwa ni mwalimu wao yaani Rabbi. Je wewe wachukua muda kuongea na Bwana na kuonja upendo wake na kujua ataka nini kwako au wakurupusha tu sala na maisha yako ya kiwito kwa ujumla kiasi kwamba huoni Bwana ni nani? Mtume Andrea anampeleka kaka yake Simon Petro kwa Yesu baada ya kujua kwamba Kristu ni Masiha, je sisi katika kutekeleza wito wetu twawapeleka ndugu zetu kwa Bwana au kwa watu wengine?

Bwana anamwambia Simoni Petro kuwa ataitwa Kefa yaani Petro au Mwamba! Anaanza kumtayarisha kwa kuwa mwamba wa Kanisa, Je, wewe uko tayari kuwa mwamba wa upendo katika familia yako na mahali pako pa kazi? Tafakari.

Mpendwa mwana wa Mungu ninakutakieni Dominika njema ukajazwe na upendo wa Bwana uwe chumvi na mwanga kwa ajili ya wengine. Kwa njia yako watu wamwone Mungu. Kwa njia ya matendo yako adilifu na unyenyekevu wako umwachie nafasi Yesu Kristo akue na hivi polepole Neema za Mungu zienee kwa wote.

Tumsifu Yesu Kristo. Kutoka katika studio za Radio Vatican ni Padre Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.