2015-01-14 08:34:20

Mtakatifu Vaz ni: Baba wa Maskini; mmissionari mahiri na mjenzi wa amani!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 14 Januari 2015, akiwa Jimbo kuu la Colombo, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kumtangaza Mwenyeheri Joseph Vaz kuwa Mtakatifu, kilele cha hija yake nchini Sri Lanka. Baba Mtakatifu wakati wa mahubiri yake, akifanya rejea kwenye Liturujia ya Neno la Mungu, amesema kwamba, mwisho wa nyakati watu wote watauona wokovu wa Mungu na kwamba, Wakristo wanaendelea kuhamasishwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa mataifa yote, kwani huu ni urithi mkubwa kwa wale wote waliotakatifuzwa na Kristo!

Baba Mtakatifu anasema, maisha ya Mtakatifu Joseph Vaz yamekuwa ni ushuhuda wa Maandiko Matakatifu mintarafu upatanisho, kiasi hata cha kujisadaka maisha yake, ili kufikia lengo hili. Ni mtakatifu aliyezaliwa Jimbo kuu la Goa, lakini akaamua kwenda nchini Sri Lanka akiwa na ari na mwamko mkuu wa kimissionari. Akatambua matatizo na changamoto zilizokuwa zinamkabili, akafanya kazi kwa uficho, lakini akajitosa kuinjilisha hata nyakati za usiku. Akawa ni chemchemi ya nguvu na moyo mkuu kwa Wakatoliki waliokuwa wanateseka kwa wakati ule!

Mtakatifu Vaz ni Padre aliyejisadaka kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa waliokuwa wamekumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa ndui katika Ufalme wa Kandy, uliosababisha majanga makubwa, kiasi cha Mfalme kumpatia ruhusa Padre Vaz kutekeleza utume wake ndani na nje ya ufalme huu pasi na kificho tena.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia mambo makuu matatu ambayo yanampatia utambulisho wa pekee Mtakatifu Vaz katika maisha na utume wake: kwanza kabisa alikuwa ni Padre aliyejisadaka kwa ajili ya wote pasi na kujibakiza; akatoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Alivumilia shida, mateso na magumu ya maisha kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu, akaonesha utii na upendo mkuu kwa Kristo na Kanisa lake; mambo makuu yaliyomletea mabadiliko ya ndani katika maisha yake.

Wakatoliki walikuwa ni kundi dogo nchini Sri Lanka, lakini lililokuwa limegawanyika na nje ya kundi hili walikabiliana na upinzani mkubwa kiasi hata cha kudhulumiwa. Padre Vaz akajishikamanisha na Kristo Msulubiwa katika sala, mtindo wa maisha na utume wake, kiasi kwamba, akawa ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Mtakatifu Vaz alikuwa ni Padre aliyetekeleza utume wake kwa ajili ya huduma ya amani, licha ya migawanyiko ya kidini iliyokuwepo. Aliwamegea na kuwashirikisha watu upendo wa Mungu katika maisha yake, akawa ni mfano bora wa kuigwa kama linavyojionesha leo hii Kanisa nchini Sri Lanka linalotaka kujipambanua kwa njia ya huduma kwa wote pasi na ubaguzi. Huduma inayotolewa katika sekta ya elimu, afya na katika matendo ya huruma. Kanisa linachoomba ni uhuru wa kutekeleza utume na dhamana yake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, uhuru wa kuabudu na kidini ni kati ya haki msingi za binadamu. Mtakatifu Vaz anawafundisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema umuhimu wa kuheshimu na kuthamini utakatifu wa maisha, utu na heshima ya kila binadamu; umuhimu wa kujikita katika kukuza na kuendeleza amani pamoja na kutafuta mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anasema, Padre Vaz alijpambanua kwa kuwa ni mmissionari mahiri, akawaonjesha watu ukarimu wa Kiinjili, katika unyofu, akakubali kuacha yote na akatambua uzuri wa Neno la Mungu mintarafu wingi wa dini, kwa heshima na majitoleo, akadumu katika fadhila ya unyenyekevu. Hii ni changamoto kwa waamini wote kuhakikisha kwamba, wanachangia katika mchakato wa kujenga na kudumisha: haki, amani na upatanisho wa kitaifa nchini Sri Lanka.

Katika salam zake kwa Baba Mtakatifu, Kardinali Malcolm Ranjith wa Jimbo kuu la Colombo, amesema, wananchi wa Sri Lanka wanajiunga na mamillioni ya watu kutoka sehemu mbali mbali kumpokea kwa heshima na mapendo makuu, kwa kuwapatia zawadi ya Mtakatifu Joseph Vaz anayeijaza mioyo yao kwa furaha kuu; kwani ni kiongozi aliyejisadaka kwa ajili ya huduma, akawa tayari kuwaimarisha Wakatoliki walipokumbana na magumu katika historia yao.

Kwa sasa Sri Lanka imeanza mchakato wa upatanisho wa kweli, haki, amani na maendeleo ya watu wake, hija ambayo ni ngumu na inahitaji neema na mwongozo thabiti, ili kutibu na kuganga madonda ya ndani, kwa kujikita katika msamaha na upatanisho, ili kweli watu waweze tena kuelewana na kukuza amani na utulivu licha ya tofauti zao za kiimani.

Mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Kardinali Ranjith amemkabidhi Baba Mtakatifu hundi ya dolla za kimarekani sabini elfu, ili ziweze kumsaidia katika kuwahudumia maskini sehemu mbali mbali za dunia! Sri Lanka hata katika umaskini wake, bado imeendelea kuonesha mshikamano wake wa upendo kwa wahitaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.