2015-01-14 10:43:08

Kulikoni?


Juma lililopita tulishuhudia kitendo cha kubatizwa mwalimu mkuu kikifuatiwa na kutambuliwa rasmi kama mtangazaji wa utawala wa mpya hapa duniani. Siku ya pili baada ya kusimikwa huko yaani leo tunawaona wafuasi wawili wanajiunga naye. Aidha kati yao, mmoja ananogewa mno na mambo, anaenda kumtonya mwingine, hadi anavutika kujiunga na msafara wa mwalimu. Hebu fuatilia kwa ukaribu mambo yalivyokuwa.

Sura ya kwanza inaanza na aya ya ishirini na tisa: “Yohane alikuwa amesimama pamoja na wawili katika wanafunzi wake”. Manzoni aya hiyo inasomeka hivi: “Tena siku ya pili yake Yohane alikuwa amesimama…,” yaani ilikuwa siku ya pili, kwa sababu siku ya kwanza Yohane alimaliza utume wake alipombatiza Yesu, akabaki bado pale Yordani. Siku hiyo ya kwanza Yohane alikuwa peke yake na Yesu tu, na alipomwona akasema: “Tazama Mwanakondoo wa Mungu…!” Yaonekana hapa Yohane anataka kutuonesha sisi sote kuwa Yesu ndiye aondoaye dhambi za dunia.

Leo siku ya pili, Yohane yuko pamoja na wanafunzi wake wawili. Anapomwona Yesu akipita njiani katika safari zake akawatonya wafuasi wake na kuonesha: “Tazameni mwanakondoo wa Mungu…” Unaalikwa kusoma kwa makini sana jinsi neno hili “kuona” lilivyotumika hapa. Siku ya kwanza lilitumika neno kwa kigiriki blepo, kwa kilatini videt, na kwa kiswahili kuna neno kuona yaani kuangalia kwa kawaida. Leo siku ya pili linatumika neno la kigiriki emblepo, kwa kilatini ni respiciens, na kiswahili kuna neno kutazama. Maana halisi ya emblepo ni “kutazama kwa makini, au kuchunguza kwa undani.”

Leo Yohane amemtazama Yesu kwa undani na amegundua hadhi na siha aliyonayo, kisha anaishuhudia hadhi hiyo na anamwita: Mwanakondoo. Yohane angeweza pia kumtambua na kumpa Yesu hadhi nyingine mathalani: mfalme, mchungaji, masiha, mshindi, rabi, nabii, mwamuzi au hata mwalimu. Lakini kumbe amechagua kumwita Mwanakondoo.

Kulikoni? Maana ya kwanza inamhusianisha Yesu na yule Mwanakondoo wa Pasaka katika kitabu cha Kutoka ambaye wayahudi walimchinja na kumla kabla ya kuanza safari yao ya kuelekea nchi ya ahadi. Damu yake ikapakwa kwenye vizingiti vya milango na kuwakinga dhidi ya nguvu za malaika wa mauti aliyepita.

Kwa hiyo Yesu ni Mwanakondoo anayejitoa mwenyewe kuwa chakula cha uzima, na damu yake inatukinga dhidi ya maovu yanayoharibu uzima. Maana nyingine ya kondoo ni ile ya kitabu cha Isaya anapomweleza “Mtumishi wa Yahwe, anayeongozwa kama kondoo kwenda kuchinjwa.” Maana yake, Yesu ataongozwa kusulibiwa. Maana nyingine ya Mwanakondoo inahusianishwa na sadaka aliyotoa Abrahamu pale mwanae Isaki anaposema: “Anakosekana kondoo wa sadaka.” Abrahamu akamjibu, “Mungu mwenyewe atamtoa kondoo, atakayejitoa mwenyewe kama sadaka.” Yesu atakufa msalabani.

Yohane mbatizaji anamnadisha huyu Yesu mara mbili kuwa ni Mwanakondoo. Hapo mwinjili Yohane anataka kutoa katekisimu (fundisho) kwa wakristu wa wakati wake, juu ya hadhi ya Yesu wa Nazareti.

Nabii Daniel anasema kuwa ufalme wa ulimwengu huu ni wa kinyama (wa kiubabe) tena ni mbwa mwitu. Ili kuubadili ulimwengu huu wa wanyama Mungu akakubali kushindwa Yeye na kujionesha kama kondoo. Akijua kwamba mbele ya kondoo, mbwa mwitu anaweza kujitambua kuwa ni mnyama mkali na siyo mpole. Ni Kondoo peke yake anayeweza kutuonesha maisha ya kiutu na ubinadamu.

Wafuasi wale wawili wakaamua kumfuata huyo Mwanakondoo. Yesu anageuka na anawaangalia wanavyomfuata kisha anawauliza: “Mnatafuta nini?” Swali hilo ni la kwanza Yesu anapoanza safari ya maisha yake hivi laonekana ni swali muhimu. Ama kweli ni muhimu kwani linaulizwa mara nyingi. Baada ya kufufuka kwake Yesu alimwulia Maria Magdalena. Kwa wafuasi hawa wawili anawauliza akitumia uwingi “Mnamtafuta nani?” na kwa Maria Magdalena aliuliza katika umoja “Unatafuta nini?” Kwa hiyo swali tungeweza kulielekeza pia kwetu binafsi: “Unatafuta nini au mnatafuta nini na kwa malengo gani?

Wengi tunamtafuta Yesu na tunategemea kutendewa muujiza fulani. Tukifanya hivyo tunafanana na Herode. Wengine tunapuyanga tu na safari yao ya maisha inakuwa bila malengo yoyote bali a ni pilikapilika. Yesu anayatambua mahangaiko yangu ya ndani, leo ananiambia “Ukitaka amani wewe nifuate mimi kwa miaka hii mitatu utapata jibu.” Wafuasi hawa hawakutosheka na ushuhuda wa Yohane, kutokana na mahangaiko waliyokuwa nayo, wakaamua kumfuata Yesu ili awaondolee dukuduku yao.

Wakamwuliza: “Hivi Bwana unaishi wapi”: Hapa isieleweke kwamba wanataka kujua anuani na mtaa anakoishi, la hasha kwani ilieleweka wakati huo Yesu hakuwa Nazareti, bali alikuwa Bethbara karibu na mahali pale alipobatizwa jana yake. Kumbe swali hili lina maana tofauti. Tungeweza kusema ni swali la mshangao kama vile pale mtu asiyejua jambo linalojulikana na watu wote anapoulizwa: “Hivi mwenzetu unaishi wapi?”

Jibu la Yesu ni “Njoni nanyi mtaona.” Wanamfuata na wanaona anapoishi huyo Mwanakondoo na huko wanapata fursa ya kutafakari sura ya Mwanakondoo, na kugundua kuwa anaishi katika fikra za Baba. Hiyo ilikuwa saa kumi jioni ndiyo saa iliyobaki katika wafuasi hawa wawili. Hiyo ni saa ya mwisho wa safari ya zamani na ni mwanzo safari mpya.

Baada ya mang’amuzi ya kukaa na Yesu, Andrea anakereketwa zaidi moyoni na hawezi kubaki na mang’amuzi hayo moyoni mwake bila ya kuyashirikisha. Ndipo anapokutana na ndugu yake Petro na kumtonya aliyoona: “Tumemwona Masiha, (maana yake, Kristo)”. Kisha anampeleka kwa Yesu, naye Yesu anamtazama akitumia neno lile lile la emblepo, au respicens, yaani kutazama kwa makini. Kwa kumtazama hivyo Yesu anaitambua hadhi ya nafsi ya Petro, anamwambia “Wewe ni Simoni, mwana wa Yohane; utaitwa Kefa (tafsiri yake Petro au jiwe).”

Toka hapo Yesu harudi tena Nazareti bali analowea huko na kwenda kuishi nyumbani kwa Petro na Andrea kule Kafarnaum. Akiwa anatokea Kafarnaumu ataendelea na safari yake ya kuteua jopo la wafuasi kama tutakavyoendelea kusikia Dominika ijayo kutoka Injili ya Marko.

Ndugu zangu, katika safari refu ukibeba chakula, huwi na wasiwasi wa kufa njaa. Katika ya maisha yetu, Tunamfuata Kondoo, na tunaalikwa kuila nyama yake na kuinywa damu yake, ndiyo komunyo takatifu. Wakati wa Misa tunaalikwa kumla Kristu na kunywa damu yake, tunaalikwa kutoa jibu la kiarusi, yaani kuunganisha maisha yetu na ya Yesu: “Huyu ndiye Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za dunia. Heri yao walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya mwanakondoo.” Yeye anajitambulisha kwetu kama Mwanakondoo na anakualika na kukuambia: “Je, unataka kuunganisha maisha yako na yangu?” Pale utakapojibu tu ndiyo, mara moja unaingia kwenye arusi ya Mwanakondoo na kuwa naye safarini. Nakutakia uamuzi bora!

Padre Alcuin Nyirenda, OSB








All the contents on this site are copyrighted ©.