Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kumtangaza
Padre Joseph Vaz kuwa Mtakatifu, Jumatano tarehe 14 Januari 2014 alielekea kwenye
Madhabahu ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu Madhu, kwa ajili ya kusali na kumshukuru
Mungu kwa matendo makuu katika maisha na utume wa Kanisa nchini Sri Lanka. Katika
madhabahu haya, wananchi na waamini wa dini mbali mbali wanajisikia kuwa nyumbani
na kwamba, hapa wanapendwa na Mama!
Tukio hili limehudhuriwa na umati mkubwa
wa watu ambao bado wanakumbuka mateso na madhulumu waliyokumbana nayo katika historia
ya nchi yao. Ibada hii imefanyika pembeni mwa Sanamu ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu
wa Madhu, iliyopelekwa nchini Sri Lanka wakati wa kupandikiza mbegu ya Ukristo.
Familia
nyingi zimeendelea kuwa na ibada kwa Bikira Maria anayewalinda wananchi wa Sri Lanka
katika shida na magumu mbali mbali, kwani daima yuko karibu na Mwanaye Mpendwa, Yesu
Kristo aliyesulubiwa, akafa na kufufuka ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi
la dhambi na mauti!
Baba Mtakatifu katika tafakari yake, anawaalika waamini
na watu wote wenye mapenzi mema kumshukuru Bikira Maria aliyewapatia zawadi ya Yesu
Kristo anayewakirimia ujasiri wa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa amani katika
mioyo yao. Baada ya chuki, kinzani, vita na uharibifu mkubwa, kuna haja ya kumshukuru
Bikira Maria, ili awakirimia daima Yesu Kristo anayeweza kuponya madonda na kuipatia
tena amani mioyo iliyovunjika na kupondeka.
Baba Mtakatifu anasema, ni pale
tu ambapo, watu wanaweza kutambua uwezo wao na jinsi ambavyo wameshiriki katika mambo
yote haya, tayari kutubu na kuomba msamaha, ili kupokea neema ya kuweza tena kukaribiana
na jirani kwa moyo wa toba ya kweli, ili kutafuta upatanisho wa kweli. Waamini wanahamasishwa
kuomba huruma na neema ya Mungu, ili kupata msamaha wa dhambi zao. Yote haya yanaweza
kufahamika kwa mwanga wa Msalaba wa Kristo unaowajalia tena neema ya kutubu na kuanza
mchakato wa upatanisho wa kweli, kama sehemu ya jitihada za kufikia amani ya kweli.
Baba Mtakatifu Francisko mwishoni anawaombea, ili Bikira Maria awasaidie
wananchi wote wa Sri Lanka kujenga na kudumisha umoja wa kitaifa, kwa kutambua kwamba,
wote ni ndugu wamoja wanaoweza kwenda nyumbani kwa Baba ili kujipatanisha sanjari
na ujenzi wa umoja na udugu.
Wakati huo huo, Askofu Joseph Rayappu wa Jimbo
Katoliki la Mannar amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwa ni hujaji na mjumbe
wa amani inayojikita katika ukweli, haki na upatanisho. Anampongeza kwa kuwajali na
kuwapenda maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mannar ni mahali ambapo
kuna Wakristo wengi waliomwaga damu yao kutokana na chuki za kidini, kiasi kwamba,
damu ya mashuhuda hawa imekuwa kweli ni mbegu ya Ukristo nchini Sri Lanka.
Madhabahu
ya Madhu yana utajiri mkubwa wa kihistoria, kwani yalijengwa zaidi ya miaka 400 iliyopita;
mahali ambapo watu walikimbilia kupata faraja wakati wa madhulumu; pakawa ni mahali
pa kukuza na kudumisha imani na ibada kwa Bikira Maria. Ni madhabahu yanayohamasisha
miito mbali mbali ndani ya Kanisa. Ni mahali ambapo umati mkubwa wa waamini unafurika
kwa ajili ya Ibada kwa Bikira Maria.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.