Hospitali ya Bambino Gesù: Prof. Profiti ang'atuka kutoka madarakani!
Professa Giuseppe Profiti, aliyekuwa Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù. inayomilikiwa
na kuendeshwa na Vatican, ameamua kung'atuka kutoka madarakani, ifikapo tarehe Mosi,
Aprili 2015. Anasema, katika kipindi cha miaka saba ya uongozi wake katika Hospitali
ya Bambino Gesù, anamshukuru Mungu kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana na kwamba,
anachukua fursa hii pia kuwashukuru na kuwapongeza wafanyakazi na wadau mbali mbali
waliowezesha Hospitali ya Bambino Gesù kupata mafanikio makubwa kiasi hiki!
Professa
Profiti anasema, umefika muda wa kuangalia kwa imani na matumaini changamoto nyingine
zilizopo katika maisha na kutoa nafasi kwa kiongozi mwingine ili kuendeleza mafanikio
pamoja na kufanya maboresho mengine zaidi. Itakumbukwa kwamba, tangu mwaka 2008 Professa
Profiti aliteuliwa kuwa Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù na tangu wakati huo kumekuwepo
na maendeleo makubwa katika huduma ya tiba na tafiti, kiasi cha kuwa ni kituo kikuu
cha tiba kwa watoto wadogo Barani Ulaya.
Hospitali ya Bambino Gesù imeendelea
kushirikiana kwa karibu na wadau wengine katika huduma ya watoto wadogo huko Cambodia,
Vietnam na Tanzania, hususan kwenye Hospitali ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Tanzania,
ambako sasa watoto waliokuwa wanalazimika kupelekwa Italia kwa ajili ya tiba ya magonjwa
ya moyo, wanaweza kutibiwa Hospitalini hapo.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.